Kafulila alitega Bunge
Ataka limtimue mbunge wa CCM
SIKU moja baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) kumshikilia Mbunge wa Jimbo la Bahi, Omary Badwel (CCM), kwa
tuhuma za rushwa, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amelipa Bunge
masharti magumu na kulitaka liyatekeleze katika mkutano ujao wa bajeti
unaoanza Juni 12.
Kafulila amelitaka Bunge, kumvua wadhifa wa ubunge, Badwel mara moja,
na pili kuivunja Kamati ya Hesabu za Serikali (LAAC) chini ya Uenyekiti
wa Augustine Mrema.
Aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, ametaka
Bunge lifanye maamuzi hayo mapema, kwa sababu, hayo ni matokeo ya
kitendo chake cha kupuuzia tuhuma nzito alizowatuhumu baadhi ya wajumbe
wa kamati hiyo, akiwemo mbunge huyo wa Bahi kwa madai ya kupokea rushwa
kutoka kwa baadhi ya watendaji.
“Ilikuwa ni Bunge la Juni 13 mwaka jana wakati nikichangia hoja ya
mpango wa maendeleo wa miaka mitano, nilitoa taarifa inayowahusu wabunge
watatu akiwemo Mbunge huyu Badwel wa kamati hiyo kutuhumiwa kwa rushwa.
“Lakini sikupewa ushirikiano toka kwa wadau wote, likiwemo Bunge
lenyewe na Tamisemi. Sasa hatimaye imedhihirika kuwa kile nilichokisema,
wakakidharau kimekuwa kweli, na ninatamka rasmi kuwa sina imani tena na
kamati hii kwa kuwa imepoteza uhalali wa kuendelea kuwa kamati ya
kusimamia na kudhibiti hesabu za serikali,” alisema Kafulila.
Kwa kuzingatia hoja hiyo, alisema sasa ni wajibu wa Spika kutafakari
upya kuhusu hadhi ya kamati na kuipanga upya kwa maslahi ya umma,
heshima na hadhi ya Bunge.
Kwa mujibu wa Kafulila, akiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya
Bunge na kwa kuwa Bunge lina mamlaka ya kumvua ubunge mbunge yeyote kwa
azimio la Bunge, anaiomba kamati kuiwasilisha hoja hiyo katika mkutano
ujao wa Bunge ili stahiki zichukuliwe kulinda heshima ya chombo hicho.
Alitahadhalisha kuwa ikiwa Spika hataona umuhimu wa kuyatendea kazi mambo hayo mawili, ajue itakuwa aibu kubwa kwa Bunge.
Alionya kuwa ikiwa hakutachukuliwa hatua kali kwa wabunge wanaopata
tuhuma, huenda siku za usoni Bunge zima likajikuta lina watuhumiwa na
hivyo kupoteza imani kwa wananchi ambao wanalitegemea katika kutoa
maamuzi makubwa na kuisimamia serikali kufanya kazi zake kwa kufuata
uadilifu.
Alitoa mfano wa Bunge la Uingereza lililowawajibisha wabunge wake
zaidi ya mara 59 na Bunge la India likafanya hivyo hivyo mwaka 1979,
hivyo haoni kwa nini Bunge la Tanzania lisuesue kuchukua hatua kama
hizo.
Alipoulizwa ni kwa nini hatua zichukuliwe kwa mbunge huyo wakati
tayari kuna wabunge wengi wanaotuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali, Kafulilia
alisema huu ni mwanzo wa kuanza ukurasa mpya, na kuacha tabia ya kusema
mbona fulani alifanya.
Mbunge Badwel alikamatwa juzi na TAKUKURU katika hoteli ya Peacock
majira ya saa 9:00 akipokea rushwa ya sh milioni 1 kutoka kwa maafisa wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mkurunga mkoani Pwani.
Chanzo:- Tanzania daima
إرسال تعليق