Simba wamchunia Kocha Cirkovic

Kocha wa Simba Milovan Cirkovic

KOCHA wa Simba Milovan Cirkovic amesema hafahamu lini atarejea nchini kukinoa kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi wanaojiandaa na michuano ya Kombe la Kagame kwa vile mpaka sasa uongozi wake umekaa kimya bila kusema lolote.
Cirkovic, raia wa Serbia yuko nchini kwake kwa mapumziko mafupi baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu Bara, ambapo aliiwezesha kutwaa ubingwa.
Kocha huyo amesema mpaka sasa Simba hawajasema lolote wala kumtumia tiketi ya ndege ili aweze kurudi nchini.
Akizungumza na Chanzo:- ( http://www.mwananchi.co.tz/ ) jana kupitia tovuti ya kijamii, Facebook Cirkovic alisema ameshangazwa na ukimya wa viongozi wake, kwani kimsingi alipaswa awe tayari yuko nchini kuiandaa timu na michuano ya Kombe la Kagame.
"Naendelea vizuri na mapumziko, lakini kufahamu ni lini nitarudi Tanzania, siwezi kusema," alisema Cirkovic.
"Labda nikuambie kwamba Simba wamekuwa kimya muda wote, nimesubiri tiketi lakini mpaka sasa hawajanitumia, sasa sijui mipango yao," aliongeza.
"Sina hakika kinachoendelea Tanzania nan siku zinakwenda timu inahitaji kuandaliwa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame," alilalama kocha huyo.
Hata hivyo, zipo taarifa za ndani kuwa Simba imeshindwa kuafikiana na kocha huyo kuhusu suala la kuongeza mkataba baada ya ule wa awali wa miezi sita kumalizika.
Ugumu huo unasemekana kusababishwa na Cirkovic mwenyewe kufuatia kuitaka Simba ipande juu zaidi kwa dau kabla ya kusaini mkataba mwingine jambo ambalo Wekundu hao wa Msimbazi wanaoonekana kutaka kulipotezea. Tulipomtafuta Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage ili azungumzie suala hilo, naye alisema:
"Hayo ni mambo ya ndani hatuwezi kuzunguzia kwenye Press(Vyombo vya habari).
"Isitoshe, hata kama akija sasa hivi atafanya kazi gani, hilo naomba tuliache kwanza," alisema Rage.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Utendaji ya Simba ilitarajia kukutana jana jioni kujadili mambo mbalimbali likiwamo suala la usajili wa wachezaji.  
Wakati huo huo; uongozi klabu ya Simba upo katika mazungumzo na kipa wa JKT Oljoro, Hamadi Waziri ili iweze kumsajili kuziba pengo la Ally Mustafa 'Barthez' aliyetimkia Yanga.
Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka kwa mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la Simba amesema kuwa, Waziri ameivutia klabu hiyo na kuna uwezekano wa kumsajili kuziba nafasi ya Barthez.

Post a Comment

أحدث أقدم