TAARIFA RASMI YA TFF KAMA ILIYOTOLEWA NA OFISA HABARI WA TFF, BONIFACE WAMBURA:
Taifa Stars imetolewa kwenye mechi za
mchujo za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kufungwa kwa penalti na
wenyeji Msumbiji (The Mambas) katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa
ulioko Zimpeto pembeni kidogo ya Jiji la Maputo.
Refa Bennett Daniel alipopuliza filimbi
ya kumaliza dakika 90 za pambano hilo timu hizo zilikuwa zimefungana bao
1-1, hivyo kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo yanayoandaliwa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mikwaju ya penalti ikatumika
kupata mshindi.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam, Februari 29 mwaka huu timu hizo
zilitoka sare ya bao 1-1.
Msumbiji ndiyo walioanza kupata bao
dakika ya 9 lililofungwa na mshambuliaji Jeremias Sitoe akiungnisha
krosi ya Elias Pelembe ambaye mabeki wa Taifa Stars walifikiri ameotea.
Stars ilisawazisha bao hilo dakika ya 89 likifungwa kwa kichwa na
Aggrey Morris kutokana na mpira wa kona uliopigwa Amir Maftah.
Mikwaju ya penalti tano tano
walioifungia Stars walikuwa Amir Maftah, Shabani Nditi na Shomari
Kapombe wakati Aggrey Morris na Kevin Yondani.
Kwa vile The Mambas nao walikosa mbili
ikabidi iongezwe penalti moja moja. Waliofunga kwa upande wa Stars
walikuwa John Bocco, Frank Domayo na Mrisho Ngassa wakati Mbwana Samata
alikosa.
Akizungumzia pambano hilo, Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana hadi dakika ya mwisho.
"Tulikuja Maputo tukijua kuwa tunatakiwa
kufunga bao, tumeweza kufunga bao ingawa katika dakika za mwisho.
Unajua linapokuwa suala la penalti chochote kinaweza kutokea, na ndivyo
ilivyokuwa," alisema Kim.
Taifa Stars itarejea nyumbani Juni 19
mwaka huu, ambapo itaaondoka hapa saa 4.40 asubuhi kwa kupitia Nairobi,
Kenya na kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa
1.50 usiku.
Kikosi kilipngwa hivi; Juma Kaseja,
Shomari Kapombe, Erasto Nyoni/John Bocco, Aggrey Morris, Kevin Yondani,
Shaabani Nditi, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Thomas Ulimwengu/Haruna
Moshi, Mbwana Samata na Mwinyi Kazimoto/Amir Maftah.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
إرسال تعليق