
1.0 UTANGULIZI:
Mkutano
wa Nane wa Bunge unatarajiwa kuanza tarehe 12 Juni, 2012 na kumaliza
shughuli zake tarehe 22 Agosti, 2012. Mkutano huu utakuwa na shughuli
mbalimbali kama vile Kiapo cha Utii kwa Waheshimiwa Wabunge wateule,
kujadili Makadirio ya matumizi na mapato ya serikali kwa mwaka wa fedha
2012/2013, Maswali kwa Waziri Mkuu na Maswali ya kawaida pamoja na
chaguzi mbalimbali ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi baada ya uteuzi wa
Mheshimiwa Rais kwa baadhi ya wabunge kuingia katika Baraza la
Mawaziri.
2.0 MUDA WA MKUTANO WA NANE WA BUNGE:
Kanuni
ya 97(1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Mwaka 2007, imeweka kiwango cha
juu cha siku zitakazotumika kwa ajili ya mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya
Serikali kuwa ni siku tano. Pia, Kanuni ya 99(1) imeweka kiwango cha
siku zisizozidi hamsini kwa ajili ya Bunge kujadili utekelezaji wa
Wizara zote za Serikali.
Hivyo
basi katika Mkutano huu wa Nane jumla ya siku nne (4) zimetengwa kwa
ajili ya kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, na jumla siku
aronbaini (40) zimetengwa kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa Bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara nyingine zote.
3.0 SHUGHULI ZA SERIKALI:
Kwa
mujibu wa Kanuni 17 (1) (d) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la
2007, Shughuli ambazo zitatekelezwa katika Mkutano huu utakaokuwa wa
siku 49 za kazi ni kama ifuatavyo:
3.1. KIAPO CHA UTII:
Kwa
mujibu wa Kanuni ya 24 ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007 na kufuatia
uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ibara ya 66 (1) (e) kutakuwa na kiapo cha Utii kwa Wabunge wateule
wafuatao:-
1. Mhe. James Francis Mbatia;
2. Mhe. Janet Zebedayo Mbene;
3. Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo; na
4. Mhe. Saada Mkuya Salum.
3.2 Miswada ya Sheria:
Miswada ya Sheria itakayosomwa kwa Mara ya Kwanza na hatua zake zote: [Chini ya Kanuni ya 83 ya Kanuni za Bunge] ni kama ifuatavyo:
· Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2012 (The Finance Bill, 2012).
· Muswada Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2012 (The Appropriation Bill, 2012).
3.3 Kujadili Bajeti:
Majadiliano
ya Bajeti ya Serikali yanaongozwa na Kanuni zilizopo katika Sehemu ya
Tisa ya Kanuni za Bunge inayohusu Utaratibu wa Kutunga Sheria kuhusu
mambo ya Fedha. Kanuni ya 96(2) inaelekeza kuwa Hotuba ya Bajeti
lazima iwasilishwe Bungeni na Waziri wa Fedha kabla ya tarehe 20 mwezi
Juni kwa kila Mwaka.
Kutokana na kanuni hiyo, Bajeti ya Serikali itasomwa siku ya alhamisi tarehe 14 Juni 2012 ambapo Nchi zote za Afrika Mashariki zitasoma Bajeti zao kama ambavyo walisha kubaliana.
Katika
siku hiyo baada ya kipindi cha Maswali, Waziri anayehusika na Mipango
atawasilisha na kusoma hotuba yake ya Hali ya Uchumi wa nchi na jioni
kuanzia saa 10.00 Waziri wa Fedha atasoma Hotuba ya Bajeti ya Serikali.
Kutokana
na Utamaduni wetu baada ya kusoma Bajeti hiyo Bunge litaahirishwa kwa
siku moja kwa lengo la kuwapatia Wabunge nafasi ya kusoma na kutafakari
Hotuba ya Hali ya Uchumi na Hotuba ya Bajeti ya Serikali na kujiandaa
kwa majadiliano yatakayoanza tarehe 18 Juni, 2012 hadi tarehe 21 Juni,
2012.
Kwa
Mujibu wa Kanuni ya 98 (2) Siku ya Alhamisi tarehe 21 Juni, 2012,
Bunge litapiga kura ya uamuzi wa Bajeti ya Serikali. Siku hii ni muhimu
sana kwa Wabunge wote kuwa Ukumbini kwa sababu kura hupigwa kwa kuita
majina.
Tarehe 22 Juni, 2012 Bunge litajadili na kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2012 (The Finance Bill, 2012). Tarehe 25 hadi 29 Juni, 2012 kwa muda wa siku tano kutakuwa na mjadala
wa Hotuba ya Waziri Mkuu juu ya utekelezaji wa Shughuli za Serikali
katika Mwaka wa Fedha unaomalizika, na matarajio ya Serikali kwa Mwaka
wa Fedha unaofuata. Mjadala wa
Hotuba za Mafungu ya Wizara nyingine utaanza tarehe 02 Julai, 2012 kwa
mtiririko kama unavyoonekana kwenye ratiba hadi tarehe 20 Agosti, 2012.
4.0 SHUGHULI NYINGINE:
4.1 MASWALI:
(i) Maswali ya Kawaida:
(Chini ya Kanuni ya 39(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007):
Itakumbukwa
kuwa, nyakati za vikao vya Bajeti, Maswali yanayowekwa kwenye orodha
ya Shughuli za Bunge ni kumi tu kwa siku za kawaida na matano siku za
Alhamisi, Hivyo, katika Mkutano huu inatarajiwa kuwa, Maswali 454
yataulizwa na kujibiwa.
(ii) Maswali kwa Waziri Mkuu:
(Chini ya Kanuni ya 38(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007):
Utaratibu
wa kumuuliza Maswali Mheshimiwa Waziri Mkuu kila Alhamisi kama
tulivyokubaliana utaendelea na inakadiriwa kuwa maswali yasiyopungua 64
yataulizwa.
4.2 UCHAGUZI WA MWENYEKITI WA BUNGE:
Kwa
mujibu wa Kanuni ya 11 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007
kutakuwa na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge ili kujaza nafasi
iliyoachwa wazi na Mheshimiwa George Boniface Simbachawene (Mb)
aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati
na Madini.
4.3. UCHAGUZI WA MJUMBE WA BUNGE LA AFRIKA:
Kwa
mujibu wa Kanuni ya 12 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007
kutakuwa na uchaguzi wa mjumbe wa Bunge la Afrika ili kujaza nafasi
iliyoachwa wazi na Mheshimiwa Stephen Julius Massele (Mb) aliyeteuliwa
na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini.
Imetolewa na :
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma
na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM
Tarehe 8, Juni, 2012
Post a Comment