TEGETE AONGEZA MKATABA WA MIAKA 2 YANGA

TEGETE AONGEZA MKATABA YANGA


MSHAMBULIAJI  Jerryson John Tegete amesaini jioni hii mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kuichezea Yanga hadi mwaka 2014, hivyo kuwakata maini Simba waliokuwa wanamnyemelea kupata saini yake.
Jerry (pichani kushoto) amesema usiku huu kwamba amesaini mkataba wa miaka miwili zaidi kuendelea kuichezea Yanga. “Nimesaini leo, mimi ni mchezaji halali wa Yanga, kweli kabla ya kusaini na hali ya mambo ilivyokuwa Yanga (migogoro) niliwahi kufanya mazungumzo na viongozi wa Simba na Azam, ilikuwa kama tunaelekea kukubaliana, ila sasa nashukuru hali imetulia klabuni, nami nimesaini leo,”alisema Tegete.  
Habari zisizo na shaka kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba Tegete ambaye amemaliza mkataba wake mwezi huu, amesaini kwa watu ambao wamepewa kazi ya kufanya zoezi la usajili, Abdallah Ahmad Bin Kleb na Seif Ahmad ‘Magari’.
Simba, baada ya kipa wao Ally Mustafa Mtinge ‘Barthez’ na beki wa kati Kelvin Patrick Yondan ‘Cotton Juice’ kusaini Yanga, ikaamua kutaka kulipa kisasi na baada ya kufanikiwa kumtia mkononi Kiggi Makassy, ikahamia kwa Tegete.
Hata hivyo, wapinzani wao hao wa jadi, wameshituka mapema na kumtia pingu mpachika mabao wao huyo, ambaye msimu uliopita haukuwa mzuri kwake.
Jerry alitua Yanga mwaka 2008, akitokea sekondari ya Makongo na haikuchukua muda kuwa tegemeo la mabao kwa timu hiyo, hususan katika mechi za watani wa jadi, ingawa msimu uliopita majeruhi yalimpunguza kasi.

Post a Comment

Previous Post Next Post