Wafungwa wauana kwa visu
JESHI la Magereza, limeingia katika kashfa nzito baada ya
nyapara mkuu wa wafungwa katika Gereza la Butimba mkoani hapa kuuawa kwa
kuchomwa visu na wafungwa wenzake juzi mchana.
Nyampara huyo aliyetajwa kwa jina moja la Kishiwa, aliuawa chumbani
kwake wakati akila chakula cha mchana, baada ya wafungwa wenzake
kumfuata na kufunga mlango, kisha kumkaba na kumchoma visu sita
shingoni, ubavuni na kifuani.
Imedaiwa kuwa wafungwa wengine walishuhudia watuhumiwa hao wakiingia
ndani mwake, kabla ya kusikia tafrani kubwa iliyowafanya wavamie chumba
hicho na kukuta mkuu wao kauawa.
Watuhumiwa hao walishambuliwa vibaya kwa kipigo na wafungwa wenzao
pamoja na baadhi ya askari magereza kiasi cha kulazimika kupelekwa
hospitali kupata matibabu.
Habari za kina kutoka ndani ya gereza hilo zilizothibitishwa na
Kamishna Mkuu wa Magereza nchini (CGP), Augustine Nanyaro na viongozi
wengine waandamizi, zilisema chanzo cha mauaji hayo ni hali ya
kutoelewana baina ya wafungwa wanaotumikia vifungo virefu.
Hata hivyo, kuna madai kwamba mauaji hayo yamechangiwa na uzembe wa
uongozi wa gereza hilo wa kushindwa kuyafanyia kazi malalamiko ya siku
nyingi ya wafungwa, yakiwemo ya ukatili, ingawa Mkuu wa Gereza, Kamishna
Masidizi (ACP), Edson Yalimo, alikwepa kukwepa kutaja kiini halisi.
Baadhi ya askari magereza ambao waliomba kuhifadhiwa majina yao,
walisema kwa muda mrefu wafungwa wamekuwa wakimtuhumu nyapara huyo kuwa
ana uongozi wa kibabe ambao unakumbatiwa na viongozi wakuu wa gereza.
“Nyapara huyo alikuwa ni kama mkuu wa gereza, chochote ambacho alikuwa
akisema ndicho kilichokuwa kikifuatwa na uongozi wa gereza,” alisema
askari mwingine.
Kwamba hata kwa nyakati tofauti walipokuja viongozi wa Makao Makuu,
Naibu Kamishana wa Magereza (DCP), John Minja, na Kamishna Mwandamizi
Msaidizi wa Magereza (SACP) Mkoa wa Mwanza, RPO Raphael Mollel, wafungwa
walitoa malalamiko yao kuhusu nyapara huyo, lakini waliishia kupigwa na
kuandikishwa maelezo.
Habari zinasema wafungwa hao walimwambia Kamanda Minja kwamba kama
hawamwondoi nyapara huyo, watafanya tukio kubwa lisilokuwa la kawaida,
ikiwemo kuua askari au nyapara mwenyewe.
“Sisi askari tunajua ni mwiko kupuuzia taarifa yoyote ya kialifu,
tunashangaa ni kwanini mkuu wa gereza na viongozi wengine walipuuzia
taarifa hizi,” alisema askari mwingine.
Mkuu wa Magereza nchini, Nanyaro, alikiri kutokea kwa tukio hilo,
lakini akasema kuwa alikuwa safarini mkoani Mbeya na hivyo ameagiza
apatiwe taarifa kamili ndipo aweze kutoa taarifa.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
إرسال تعليق