MWENYEKITI wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA), jana aligeuka
mbogo na kuwafukuza watendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori
Nchini (Tawiri) baada ya kubaini kupotea kwa silaha ambazo hadi sasa
hazijulikani ziliko.
Zitto akiungwa mkono na wajumbe wa kamati hiyo, alisema kamati hiyo
imepata hofu kubwa juu ya kutoweka kwa bunduki hizo, na zaidi baada ya
kubainika kuwa moja ya silaha zinazoaminika kumilikiwa na taasisi hiyo
kuhusishwa na tukio la mauaji mjini Mugumu, mkoani Mara.
Mbali na kuwafukuza watendaji wa taasisi hiyo, aliwaagiza kuwasilisha
haraka ndani ya wiki mbili, ripoti kamili itakayoeleza kinagaubaga namna
silaha hizo aina ya bunduki zilivyotoweka katika mazingira ya
kutatanisha tangu mwaka 1980.
Zitto alisema kuwa suala la upotevu wa silaha hizo, na nyingine
kuhusika katika matukio ya kihalifu ni nyeti, na hivyo kamati hiyo ya
Bunge inahitaji maelezo ya kina kutoka kwa watendaji hao, hivyo
akawatimua, na kuwaagiza wawasilishe kwake ripoti ya kina mjini Dodoma
wakati wa mkutano wa bajeti unaotazamiwa kuanza Juni 12, mwaka huu.
“Sisi kama kamati tumeamua kutoendelea kuijadili taarifa hii kutokana
na kuwa na hofu na suala hilo kwani hivi sasa kuna taarifa ya silaha
yenu namba 00980 ambayo inashikiliwa katika kituo cha polisi Mugumu
tangu mwaka 1999 baada ya kudaiwa kutumika kwenye mauaji,” alisema
Zitto.
Mwenyekiti huyo alishangazwa na kitendo kilichoonyeshwa na taasisi
hiyo cha kushindwa kufuatilia zilipo silaha hizo jambo ambalo linatoa
taswira kuwa zinaweza kuwa zinatumika katika uhalifu unaojitokeza
nchini.
Alisema silaha hizo zinazomilikiwa na tawi la utafiti la Kingupira
lililoko mbuga za wanyama za Serous ziligundulika kutokuwepo katika
kituo hicho baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa mwaka 2008 na 2009.
Zitto alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida na inayotia mashaka,
watendaji wa taasisi hiyo hadi sasa hawajatoa taarifa polisi kuhusu
kutoonekana silaha hizo kwa kipindi chote hicho.
“Ninachofahamu ni kuwa kama silaha yako haionekani kitu cha kwanza ni
lazima utaarifu vyombo vya dola …lakini ninyi wenzetu mmenyamaza kimya
wala hamjawa na hofu na suala hilo,” alisema.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM), alitaka kujua kwa nini baada ya
mkaguzi kugundua suala hilo limechukua muda mrefu bila kushughulikiwa.
“Hivi mnafahamu unyeti wa suala hili? Mnajua kwa sasa nchi yetu iko
katika wakati gani katika suala la uhalifu? Sio katika maeneo ya mijini
tu bali hadi katika hifadhi zetu wanyama wengi wanauliwa hovyo.
Inawezekana silaha hizo ndizo zinatumika,” alisema Lugora.
Akijitetea Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, Paul Sarakikya,
alisema kuwa hawajalipeleka suala hilo polisi kutokana na wizara kuanza
kufanya uchunguzi.
Alimuomba mwenyekiti wa kamati hiyo kuwapa mwezi mmoja ili kukamilisha uchunguzi huo jambo ambalo halikuafikiwa.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Simon Mduma, alisema kuwa kutokana na
uzito wa suala hilo Aprili mwaka huu walilazimika kuiandikia Wizara ya
Maliasili na Utalii barua na kuhoji ziliko silaha hizo kwa kuwa hata
katika vitabu vyao hakukua na taarifa zozote.
Post a Comment