Uchunguzi vibali bandia wakamilika

TUME iliyoundwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kuchunguza utoaji wa vibali bandia kwa raia wa kigeni imemaliza kazi yake huku baadhi ya maofisa wakishindwa kujua hatma yao.
Tume hiyo chini ya uenyekiti wa Augustino Shio ilihitimisha uchunguzi wake kwa kuwahoji baadhi ya maofisa waandamizi akiwemo DCI Zubeda Mjaga.
DCI Mjaga anatuhumiwa kuwa na akaunti ya fedha za kigeni katika benki ya CRDB tawi la Moshi zinazodaiwa zimetokana na utoaji wa vibali bandia kwa raia wa kigeni.
Mwenyekiti huyo alizungumza na Tanzania Daima juzi na kusema tume yake ilitembelea taasisi 14 ambapo vibali hivyo vilitolewa zikiwamo hoteli za kitalii, viwanda na hospitali zinazoendeshwa na taasisi za dini.
Kwa mujibu wa Shio, jumla ya vibali bandia 480 vilitolewa na maofisa uhamiaji mkoani hapa kwa wageni walioingia nchini na kufanya kazi kwenye maeneo tofauti.
Habari kutoka ofisi ya uhamiaji mkoani hapa zinadai kuwa baadhi ya maofisa wanaodaiwa kuguswa na kadhia hiyo wameanza kushutumiana.
Inadaiwa kwamba vibali vinavyotolewa daraja C vinavyotakiwa kulipiwa dola 550 za Marekani vililipiwa dola 200 na kuisababishia serikali hasara ya sh milioni 231.
Licha ya hasara hiyo, serikali ilipata hasara ya sh milioni 86 kutokana na vibali bandia 84 vya daraja B vilivyokamatwa mwaka jana katika kiwanda cha Kilimanjaro Biochem kilichoko Kifaru wilayani Mwanga.
Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa habari za uchunguzi mkoani Kilimanjaro umebaini kuwa raia wa kigeni wanaolipa dola 200 badala ya 550 kila mmoja hawapewi nakala ya vibali hivyo bali hugongewa mhuri katika hati zao za kusafiria. Tume hiyo pia iliwahoji waandishi wa habari wawili.

Post a Comment

Previous Post Next Post