TUME iliyoundwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kuchunguza utoaji wa
vibali bandia kwa raia wa kigeni imemaliza kazi yake huku baadhi ya
maofisa wakishindwa kujua hatma yao.
Tume hiyo chini ya uenyekiti wa Augustino Shio ilihitimisha uchunguzi
wake kwa kuwahoji baadhi ya maofisa waandamizi akiwemo DCI Zubeda Mjaga.
DCI Mjaga anatuhumiwa kuwa na akaunti ya fedha za kigeni katika benki
ya CRDB tawi la Moshi zinazodaiwa zimetokana na utoaji wa vibali bandia
kwa raia wa kigeni.
Mwenyekiti huyo alizungumza na Tanzania Daima juzi na kusema tume
yake ilitembelea taasisi 14 ambapo vibali hivyo vilitolewa zikiwamo
hoteli za kitalii, viwanda na hospitali zinazoendeshwa na taasisi za
dini.
Kwa mujibu wa Shio, jumla ya vibali bandia 480 vilitolewa na maofisa
uhamiaji mkoani hapa kwa wageni walioingia nchini na kufanya kazi kwenye
maeneo tofauti.
Habari kutoka ofisi ya uhamiaji mkoani hapa zinadai kuwa baadhi ya
maofisa wanaodaiwa kuguswa na kadhia hiyo wameanza kushutumiana.
Inadaiwa kwamba vibali vinavyotolewa daraja C vinavyotakiwa kulipiwa
dola 550 za Marekani vililipiwa dola 200 na kuisababishia serikali
hasara ya sh milioni 231.
Licha ya hasara hiyo, serikali ilipata hasara ya sh milioni 86
kutokana na vibali bandia 84 vya daraja B vilivyokamatwa mwaka jana
katika kiwanda cha Kilimanjaro Biochem kilichoko Kifaru wilayani Mwanga.
Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa habari za uchunguzi
mkoani Kilimanjaro umebaini kuwa raia wa kigeni wanaolipa dola 200
badala ya 550 kila mmoja hawapewi nakala ya vibali hivyo bali hugongewa
mhuri katika hati zao za kusafiria. Tume hiyo pia iliwahoji waandishi wa
habari wawili.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
إرسال تعليق