KLABU ya Yanga imewatupia virago beki wake wa kulia na nahodha, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ na Abuu Ubwa, imefahamika.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake makutano
ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, jijini Dar es Salaam zinasema, nyota
hao wameachwa kutokana na kushuka viwango.
Chanzo cha uhakika kimedokeza kuwa kushuka kwao kiwango kuliwafanya
washindwe kutoa mchango uliotarajiwa kutoka kwao katika msimu uliopita
wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyofikia tamati Mei 6.
Yanga chini ya Kocha wake Mserbia, Kostadin Papic ilimaliza ligi hiyo
kwa kushindwa kutetea ubingwa wake, ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya
Simba
na Azam FC.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa, kuachwa kwa nyota hao, ni sehemu ya
mkakati wa kukisuka upya kikosi cha timu hiyo kuelekea vita ya kutetea
ubingwa wa Kombe la Kagame na msimu mpya wa Ligi Kuu.
Mbali ya kiwango, pia kiongozi huyo amedokeza kuwa, walikerwa na utovu
wa nidhamu wa ndani na nje ya uwanja wa Nsajigwa aliyekuwa nahodha wa
timu
ya soka ya Tanzania, Taifa Stars.
“Tumedhamiria kuwa na kikosi bora, sio bora kikosi kwenye ligi kuu
ijayo na michuano mingine, hivyo hatuwezi kuwa na wachezaji walioshuka
viwango,
pia nidhamu mbovu,” alisema kiongozi huyo.
Alidokeza kuwa, kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kusaka nyota bora
ambao wataziba nafasi za wale watakaoachwa kwa lengo la kujenga kikosi
bora cha ushindani.
Mbali ya Nsajigwa na Ubwa, nyota wengine walio kwenye hatari ya kutemwa,
ni Shamte Ally, Bakari Mbegu na Kiggi Makasy kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo kushuka viwango.
Kuachwa kwa Nsajigwa kunakuja huku kukiwa na habari za Yanga kuanza
kusaka saini za nyota kadhaa wakiwemo Uhuru Seleman, Juma Jabu na Juma
Nyoso kwa lengo la kuimarisha kikosi cha msimu ujao.
Shadrack, ni kati ya mabeki shupavu nchini akijaaliwa uwezo wa pumzi kiasi
cha kupanda kwenda kusaidia mashambulizi na kushuka kuzuia, akifananishwa
na lori aina ya Fuso ambalo hutumika kubeba mizigo.
Kabla ya kutua Yanga mwaka 2006 akitokea timu ya Moro United, Nsajigwa
aliwahi kuichezea Prisons ya Mbeya kwa mafanikio kama ilivyokuwa kwa
rafiki yake, kipa Ivo Mapunda aliyehama naye Moro Utd hadi Yanga.
Katika mechi ya mwisho ya kufunga Ligi Kuu dhidi ya Simba iliyopigwa
Mei 6
kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Nsajigwa alionekana
kupwaya, akisababisha penalti tatu kutokana na kucheza rafu dhidi ya
Emmanuel Okwi.
إرسال تعليق