Hali ya afya ya Dk. Steven Ulimboka ambaye anatibiwa Afrika Kusini, imebadilika ghafla na kuna habari kuwa yuko mahututi.
Habari zilizoifikia Tanzania Daima kutoka vyanzo mbalimbali vya habari
ndani na nje ya nchi, zimesema kuwa Dk. Ulimboka alikuwa amepoteza
fahamu, na juhudi za kuokoa maisha yake zilikuwa zikiendelea chini ya
jopo la madaktari bingwa wa nchi hiyo na wale wa Tanzania.
Inadaiwa kwamba hali ya kiongozi huyo wa jumuiya ya madaktari nchini
ambaye alikimbizwa nchini humo wiki iliyopita, awali ilielezwa kuwa
inaendelea vema, lakini ghafla ikabadilika na kufikia kiwango cha
kupoteza fahamu.
Mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC)
alikaririwa akisema kuwa hali ya Ulimboka ilikuwa mbaya, na kwamba
kulikuwa na ulinzi na usiri mkubwa kuhusiana na hali hiyo.
Jijini Dar es Salaam, mmoja wa madaktari aliyezungumza na gazeti hili
kwa sharti la kutotajwa jina, alisema kuwa walipata taarifa za kuzidiwa
kwa Dk. Ulimboka kutoka kwa ndugu yake aliyeko Afrika Kusini kwamba
alikuwa yuko kwenye hali mbaya, hali iliyowachanganya mno.
Mmoja wa madaktari alikiri kupokea taarifa za kuzidiwa kwa mwenyekiti wao kutoka kwa kaka wa Dk. Ulimboka.
“Leo asubuhi baada ya kupokea taarifa za kuzidiwa kwa Dk. Ulimboka
kikaitishwa kikao cha dharura cha madaktari wote tunaelekea huko,”
alisema.
Hata hivyo, majira ya mchana habari zilivuma kwamba Dk. Ulimboka
alikuwa amefariki, hali iliyozidi kuzusha wasiwasi mwingi miongoni mwa
madaktari, viongozi wa vyama vya kijamii na wananchi wa kawaida
waliokuwa wakihaha kupata ukweli wake.
Uvumi huo hata hivyo, ulikanushwa baadaye na msemaji wa Hospitali ya
Muhimbili Kitengo cha Mifupa MOI Almasi Jumaa lakini akakiri kupata
taarifa za kubadilika kwa hali ya mgonjwa huyo.
Chanzo:- Tanzania Daima
Post a Comment