MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda anayekipiga katika timu ya Simba
ya Tanzania, Emmanuel Okwi, amesema hana mpango wa kujiunga na timu
nyingine nchini isipokuwa kucheza soka barani Ulaya.
Okwi amesema, hata kama mipango ya kucheza Ulaya itakwama, hatajiunga
na timu nyingine nchini zaidi ya kuendelea kuitumikia Simba.
Akizungumza kwa simu kutoka nchini Uganda jana mchana, Okwi alisema
anatarajia kuondoka nchini Uganda siku yoyote kwenda nchini Italia kwa
majaribio kwenye klabu ya Parma iliyo Seria A.
Nyota huyo aliyezaliwa Desemba 25, 1992, alisema kabla hajafanikiwa Ulaya, yeye ni mali ya Simba,
hivyo viongozi na mashabiki wasiwe na hofu.
“Ninashangazwa kuwepo taarifa kuwa nimejisajili
na Yanga, mimi nipo hapa Uganda na leo hii (jana), natarajia kupata viza ya kuniwezesha kwenda Italia kwa majaribio,” alisema.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema Okwi bado ni mchezaji
wao, mkataba wake utafikia tamati mwaka 2013.
Kaburu amewasihi wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hiyo,
kutokuwa na hofu juu ya mchezaji huyo anakwenda Italia kwa majaribio kwa
baraka zao.
“Okwi ni kati ya nyota wenye uelewa mkubwa akitambua thamani na wajibu
wake, hawezi kufanya mambo kama hayo yanayosambazwa kwa simu,” alisema
Kaburu.
Kaburu alisema Okwi na beki wao Kelvin Yondan aliyejiunga Yanga, ni
kati ya wachezaji wenye mikataba, hivyo kuhitaji mazungumzo kabla ya
kuwachukua.
Alisema mbali na majaribio ya Italia ambayo kwa asilimia kubwa
yatamuwezesha kujiunga nayo, Okwi pia amepata ofa nchini Ujerumani,
Etoile Du Tunisia ya Tunisia, Mamelod Sundows na Orlando Pirates za
Afrika Kusini.
Okwi ni kati ya wachezaji waliotoa mchango mkubwa kwa timu ya Simba
kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara hadi kutwaa tuzo ya nyota
bora wa kigeni
Post a Comment