• Viongozi wa dini kuwakutanisha madaktari na JK
HALI ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari hapa nchini, Dk. Stephen
Ulimboka, inazidi kuzorota na madaktari walio karibu naye wamedokeza , kuwa sasa wanasubiri ‘Kudra’ za Mwenyezi Mungu’
Kiongozi huyo ambaye alitekwa, kuteswa na kutupwa katika msitu wa
Mabwepande jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita anatibiwa
katika hospitali moja nchini Afrika Kusini ambayo hadi sasa haijawekwa
wazi.
Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema
kiongozi huyo aliyelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi yumo katika
‘koma’, ambayo ni hali ya nusu mfu - nusu hai, na anahitaji zaidi sala
za Watanzania.
“Huwezi kusema anaendelea vizuri, jambo muhimu hapa ni kumwomba Mungu
awaongezee maarifa madaktari wale ili kupigania uhai wa mwenzetu.
“Kwa hali aliyoondoka nayo hapa nchini na jinsi tunavyopokea taarifa
kutoka huko, kwakweli hazileti matumaini,” alisema Dk. huyo.
Dk. Ulimboka inadaiwa amepata madhara makubwa katika figo zake ambapo
ilidaiwa moja ilipata ufa na nyingine iligoma kufanya kazi, baadhi ya
mbavu zake zimepata majeraha.
Kichwa cha daktari huyo pia kilipata hitilafu kutokana na kipigo hicho
kinachodaiwa kufanywa na maofisa Usalama wa Taifa ingawa serikali
imekana kuhusika na kitendo hicho cha kinyama.
Baadhi ya madaktari waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili jana
jijini Dar es Salaam katika mkutano na viongozi wa dini wamesema ukweli
wa kipigo cha kiongozi huyo hautawekwa wazi.
Walibainisha kuwa hawana imani na tume itakayoundwa au iliyoundwa
kushughulikia jambo hilo kwa sababu tayari viongozi wa serikali wamesema
serikali haihusiki.
“Rais, waziri wamesema serikali haihusiki na tukio hili, sasa kama
tume ikibaini kuna mkono wa serikali ukweli utawekwa wazi hapo?” alihoji
mmoja wa madaktari.
Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na Rais wa Chama cha Madaktari
Tanzania, Namala Mkopi, kuhusu afya ya Dk. Ulimboka ambapo aligoma
kuzungumzia suala hilo.
Dk. Mkopi alisema jana walikuwa kwenye mazungumzo na viongozi wa dini kuhusu mgomo wa madaktari na si vinginevyo.
Viongozi wa dini waingilia
Wakati hali ya Dk. Ulimboka ikizidi kuwa tete, viongozi wa dini
nchini wamemtaka Rais Jakaya Kikwete akutane nao pamoja na madaktari ili
kuupatia ufumbuzi mgomo wa madaktari.
Viongozi hao walisema mgomo wa madaktari unaoendelea hivi sasa unawatesa wananchi wasio na hatia.
Kauli ya viongozi hao wa dini ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na
Sheikh Said Mwaipopo mara baada ya kikao chao na madaktari.
Sheikh Mwaipopo alisema wamechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa
serikali inasuasua kulizungumzia jambo hilo kwa makini na kulipatia
ufumbuzi ili kuokoa maisha ya watu wa kipato cha chini wanaotegemea
hospitali za serikali.
“Kuna mambo mbalimbali yanaweza kutokea, inawezekana taarifa sahihi
hazimfikii Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, hivyo tunaomba kukutana
naye kwa mazungumzo ya amani ili kurudisha hali ya amani nchini,”
aliongeza Mwaipopo.
Sheikh Mwaipopo alifafanua kuwa tamko lao limejigawa katika sehemu
kuu tano, ambapo wanaamini kukutana huko kunaweza kuwa ishara ya
kumaliza mgogoro unaowakabili na kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.
Alisema miongoni mwa mambo waliyoazimia ni kuitaka serikali ifute kesi
iliyoifungua Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ambayo ilitoa zuio la mgomo
huo.
Aliongeza kuwa pia wameitaka iwarejeshe madaktari wote walioachishwa
kazi pamoja na Rais Kikwete akubali kukutana na viongozi wa dini,
wanaharakati wa haki za binadamu na madaktari.
Naye Mchungaji wa EAGT Mabibo, Lawrence Mnzavaz, alisema hawahusiki na
tuhuma zinazovumishwa kuhusu tukio lililotokea la Dk. Ulimboka, kwa
sababu hakuna aliyeshuhudia uovu huo unavyofanyika.
Alisema tamko lao halitakubaliana na kauli ya aina yoyote
itakayowataka wananchi kuandamana, kwani wanaamini hiyo si njia sahihi
ya kumaliza tatizo lililopo.
Kiongozi huyo alisema iwapo rais atashauriwa vibaya na kukataa
kukutana na umoja wa viongozi hao, hawatakuwa na la kufanya kwa sababu
maamuzi hayo yatakuwa yamefanywa na kiongozi wa nchi
Chanzo:- Tanzania Daima Jumapili
Post a Comment