Huduma za matibabu MOI zasimama tena
Taarifa za kutatanisha kuhusiana na hali ya Dk. Ulimboka,
zilisababisha kusitishwa kwa huduma za matibabu katika Kitengo cha
Mifupa cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) baada ya madaktari
karibuni wote kwenda katika mkutano wa dharura kujadili tukio hilo.
Habari za kuaminika kutoka MOI, zimethibisha kuwa taarifa za kuzidiwa
na hata kuzuka kwa habari nyingine kwamba Dk. Ulimboka alikuwa
amefariki, ziliwachanganya kwa kiasi kikubwa madaktari hao, ambao
walilazimika kusitisha huduma na kuwapangia wagonjwa tarehe nyingine za
kurudi.
Kutokana na hatua hiyo ya madaktari, wagonjwa waliofika MOI baada ya
kusikia kwamba huduma zimerejea, walishindwa kupata tiba badala yake
waliandikishwa majina, wakalipia na kupewa tarehe ya kurudi kwa madai
kwamba hakuna madaktari wa kuwahudumia.
Taarifa ya kurejea kwa madaktari hao ilitolewa juzi hospitalini hapo
jana na Mwenyekiti wa Bodi ya MOI Balozi Charles Mtalemwa na kusisitiza
kwamba hospitali hiyo haiko katika mgomo kwa sasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wagonjwa waliokosa tiba,
walidai kuchoshwa na usumbufu huo huku wakiwaomba madaktari hao kurejea
kazini.
“Nimekuja hapa tangu saa moja kulikua na foleni; wenzetu waliowahi
walionana na madaktari lakini ilipofika saa nne tukaambiwa wote
tuliojiandikisha turudi Alhamisi ijayo kwa sababu madaktari wanaenda
kwenye kikao,” alisema Abdallah Haji mkazi wa Kimara.
Kwa upande wake Jenipher Suka alisema inasikitisha kuona hivyo kwa
sababu mama yake ambaye ni mgonjwa mkazi wa Dodoma amekuja akitegemea
kupata tiba matokeo yake ameambiwa arudi tarehe 10 mwezi huu kwa kuwa
hakuna madaktari kwa sasa.
“Kwa nini serikali isiseme ukweli maana tunahangaika kuja mpaka huku
halafu hakuna huduma? Vyombo vya habari vimetangaza kwamba mgomo
umesitishwa lakini bado wanatudanganya wananchi kwa faida ya nani?”
alilalamika Jenipher.
Akizungumza kwa sharti la kutochapisha jina lake gazetini mmoja wa
maofisa waandamizi wa hospitali hiyo alikiri kutokuwepo kwa huduma baada
ya madaktari kupokea taarifa za kuzidiwa kwa Dk. Ulimboka.
“Unajua huduma zinazoendelea kwa sasa ni kliniki na upasuaji kwa
waliowahi lakini hawa madaktari wamechanganyikiwa baada ya daktari
mwenzao aliyeongozana na Dk. Ulimboka kuwaeleza kwamba hali ya mgonjwa
ni mbaya mno.
Kukosekana kwa huduma kulichangiwa na madaktari wanafunzi ambao
hupokea na kuwahudumia wagonjwa kuwa katika maandalizi ya mitihani ya
mwisho wa mwaka itakayoanza Jumatatu ya Julai 9, 2012 hivyo kusababisha
huduma utoaji wa huduma kutokuwepo kabisa.
Pinda abanwa
MJINI Dodoma, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameshindwa kuliambia Bunge
endapo serikali iko tayari kuunda tume huru kuchunguza tukio la kutekwa
na kupigwa kwa Dk. Ulimboka.
Waziri Mkuu Pinda, alishindwa kutoa kauli wakati akijibu swali la
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (CHADEMA).
Katika swali lake la nyongeza, Mbowe alisema kumekuwa na ongezeko la
vitendo vya mauaji yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alitolea mfano wa tukio la kupigwa
kwa wabunge wawili wa CHADEMA mkoani Mwanza na tukio la hivi karibuni la
kutekwa na kupingwa kwa Dk. Ulimboka.
“Kwa kuwa kumekuwa na ongezeko la matukio ya mauaji kwa raia wasio na
hatia na kumekuwa na hisia kwamba matendo hayo yanafanywa na Jeshi la
Polisi. Mfano wa matukio hayo ni pamoja na lile la kupigwa kwa wabunge
wawili na hili la hivi karibuni la kutekwa kwa Dk. Ulimboka, tukio
ambalo limelichafua taifa; je, serikali iko tayari kuunda tume huru
kuchunguza matukio hayo?” alihoji Mbowe.
Akijibu swali hilo, Pinda kwanza alisema sio kweli kwamba tukio la kupigwa kwa Dk. Ulimboka limechafua sifa nzuri ya taifa.
“Mh. Mbowe, kwanza tukio la Ulimboka sio mfano mzuri sana kwa sababu
hakuna mwenye ushahidi wa serikali kuhusika kumteka na kumpiga Dk.
Ulimboka.
“Kama nilivyosema awali, sioni sababu ya serikali kuhusika na kipigo
cha Ulimboka ambaye tulikuwa tukishirikiana naye vizuri kwenye vikao vya
majadiliano,” alisema Pinda.
Hata hivyo katika kujibu swali hilo, Pinda hakusema chochote kuhusu
swali la Mbowe aliloitaka serikali kuunda tume huru kuchunguzwa tukio la
Dk. Ulimboka.
Badala yake alisisitiza kuwa serikali itafanya uchunguzi wa kina kubaini waliohusika kumipiga Dk. Ulimboka.
Akijibu swali la msingi la Mbowe aliyehoji utekelezaji wa sheria ya
uchunguzi wa vifo vyenye utata, Waziri Mkuu Pinda alikiri kuwa mwaka
jana aliahidi Bungeni kwamba serikali ingelikuja na sheria ya uchunguzi
wa vifo vyenye utata ili kuharakisha matokeo ya uchunguzi huo.
Alisema serikali bado inaendelea na mchakato wa kuandaa sheria hiyo ili ianze kutumika.
Mbowe alisema kumekuwa na kasi ya ongezeko la vifo vyenye utata vya
raia wasio na hatia na vyombo vya dola, hasa polisi wamekuwa
wakihusishwa na vifo hivyo.
Alisema kuwa Waziri Mkuu Pinda alikiri kuwapo na hali hiyo na kuahidi
kuwa serikali ingekuja na sheria ya kuchunguza vifo vya aina hiyo.
Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu
mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika msitu wa Pande, nje kidogo ya
jiji Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi limeunda jopo kuchunguza tukio la utekaji nyara na shambulio la kudhuru mwili wa Dk. Ulimboka.
Tangu kuibuka kwa tukio hilo, wabunge mbalimbali kwa nyakati tofauti
wamekuwa wakiibua hoja ya mgomo wa madaktari na kipigo cha Ulimboka,
lakini kiti cha Spika kimekuwa kikizima kwa hoja kuwa jambo hilo liko
mahakamani.
Post a Comment