SAKATA la meli zinazohisiwa kuwa ni za Iran kupeperusha bendera ya
Tanzania limeingia katika sura mpya baada Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ) na Tanzania Bara kuamua kufanya uchunguzi utakaothibitisha
mmiliki halisi wa meli hizo.
Uchunguzi huo utafanywa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU),
Marekani na Umoja wa Mataifa (UN) ili kubaini kizungumkuti cha suala
hilo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema kuwa endapo uchunguzi
huo utabaini meli hizo ni za Iran watazifutia usajili na kuziondoa.
Membe alisema kuwa wizara yake ilimwita Balozi wa Iran, Mohsen
Movahhed Ghomi, mnamo Julai 2 mwaka huu na alikataa Iran kumiliki meli
hizo.
Aidha Membe alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilimtaka
wakala wa meli hizo Philtex Corporation kuwaita wamiliki halisi wa meli
hizo na kuwataka kujieleza kuhusiana na uhusiano wao na serikali au
makampuni ya mafuta ya Iran ambapo wameeleza kuwa hawana uhusiano wowote
na nchi. Badala yake walidai waliamua kuja kusajili meli zao kupitia
Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kwa ridhaa yao na kwa kufuata
matangazo ya usajili wa nje.
Membe pia alisema kuwa ipo sheria ya kimataifa inayozikataza nchi
mshirika kutoisaidia Iran ambayo imewekewa vikwazo ikiwa ni pamoja na
uamuzi wa Marekani juu ya ukiukaji wa vikwazo dhidi ya Iran kama
watakuwa wanaisaidia nchi hiyo kukwepa vikwazo vya kiuchumi ambavyo
vitaisaidia nchi hiyo kubadili tabia ya kuhatarisha dunia.
“SMZ na Tanzania hazitaki kupuuzia taarifa hizo za meli za Iran
kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye maji marefu ya bahari, hivyo
tutafanya uchunguzi kubaini ukweli wa jambo hilo na kama kutakuwa na
ukweli suala hili litamalizwa bila kuleta mtafaruku kwani
linazungumzika,” alisema Membe.
Akizungumzia suala la mbunge wa Marekani Howard Berman kuiandikia
Ikulu barua, Membe alisema kuwa hajui kama barua imeshafika ila wao
wanafanya hivyo kutokana na kubanwa na baraza la usalama la Umoja wa
Mataifa.
Akijibu swali lililomtaka kueleza kama SMZ inamjua mmiliki halisi,
Membe alidai kuwa Zanzibar haijui, na ndio maana wanafanya uchunguzi
kubaini mmiliki halisi ni nani, na majibu ya uchunguzi huo yatatolewa
muda wowote.
Iran imewekewa vikwazo hivyo na Marekani na EU ili isipate mapato
zaidi ya kugharamia mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia na
kusaidia ugaidi wa kimataifa
Post a Comment