Meli za Iran zaisulubu serikali

SAKATA la meli zinazohisiwa kuwa ni za Iran kupeperusha bendera ya Tanzania limeingia katika sura mpya baada Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Tanzania Bara kuamua kufanya uchunguzi utakaothibitisha mmiliki halisi wa meli hizo.
Uchunguzi huo utafanywa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), Marekani na Umoja wa Mataifa (UN) ili kubaini kizungumkuti cha suala hilo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema kuwa endapo uchunguzi huo utabaini meli hizo ni za Iran watazifutia usajili na kuziondoa.
Membe alisema kuwa wizara yake ilimwita Balozi wa Iran, Mohsen Movahhed Ghomi, mnamo Julai 2 mwaka huu na alikataa Iran kumiliki meli hizo.
Aidha Membe alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilimtaka wakala wa meli hizo Philtex Corporation kuwaita wamiliki halisi wa meli hizo na kuwataka kujieleza kuhusiana na uhusiano wao na serikali au makampuni ya mafuta ya Iran ambapo wameeleza kuwa hawana uhusiano wowote na nchi. Badala yake walidai waliamua kuja kusajili meli zao kupitia Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kwa ridhaa yao na kwa kufuata matangazo ya usajili wa nje.
Membe pia alisema kuwa ipo sheria ya kimataifa inayozikataza nchi mshirika kutoisaidia Iran ambayo imewekewa vikwazo ikiwa ni pamoja na uamuzi wa Marekani juu ya ukiukaji wa vikwazo dhidi ya Iran kama watakuwa wanaisaidia nchi hiyo kukwepa vikwazo vya kiuchumi ambavyo vitaisaidia nchi hiyo kubadili tabia ya kuhatarisha dunia.
“SMZ na Tanzania hazitaki kupuuzia taarifa hizo za meli za Iran kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye maji marefu ya bahari, hivyo tutafanya uchunguzi kubaini ukweli wa jambo hilo na kama kutakuwa na ukweli suala hili litamalizwa bila kuleta mtafaruku kwani linazungumzika,” alisema Membe.
Akizungumzia suala la mbunge wa Marekani Howard Berman kuiandikia Ikulu barua, Membe alisema kuwa hajui kama barua imeshafika ila wao wanafanya hivyo kutokana na kubanwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Akijibu swali lililomtaka kueleza kama SMZ inamjua mmiliki halisi, Membe alidai kuwa Zanzibar haijui, na ndio maana wanafanya uchunguzi kubaini mmiliki halisi ni nani, na majibu ya uchunguzi huo yatatolewa muda wowote.
Iran imewekewa vikwazo hivyo na Marekani na EU ili isipate mapato zaidi ya kugharamia mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia na kusaidia ugaidi wa kimataifa

Post a Comment

أحدث أقدم