SIKU moja baada ya viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu kujitosa
katika sakata la mgogoro wa madaktari wakishauri Rais Jakaya Kikwete
akutane na madaktari pamoja na viongozi hao ili kutafuta ufumbuzi wa
mgogoro wao unaoendelea, Ikulu imejibu ikisema kuwa hawana sababu ya
kupitia kwa watu wengine kuomba kukutana na viongozi wa serikali.
Juzi viongozi hao walikutana na Jumuiya ya Madaktari na wanaharakati
jijini Dar es Salaam jana katika harakati za kujaribu kuwasihi wasitishe
mgomo ili kuwanusuru wananchi na hivyo kupendekeza kuwa iundwe kamati
huru ya kuchunguza tukio la kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, mapema iwezekanavyo ili kupata ukweli wa
kilichotokea.
Dk. Steven Ulimboka, yuko nchini Afrika Kusini kwa matibabu baada ya
kutekwa na kupigwa na watu wasiojulikana, tukio ambalo lilifanyika siku
chache baada ya madaktari hao kuanza mgomo.
Akisoma tamko la viongozi hao, Mkurugenzi wa Baraza la Habari la
Kiislamu (Bahakita), Hussein Msopa, kwa niaba ya viongozi hao, alisema
kwamba kuundwa kwa kamati huru ya uchunguzi kutasaidia kupata ukweli wa
tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk. Ulimboka na kuwezesha kubaini
wahusika wa tukio hilo.
“Tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande Dk.
Ulimboka ni la kusikitisha… na tunamuomba Rais Kikwete aunde tume huru
itakayojumuisha madaktari wenyewe, viongozi wa dini, wanaharakati na
wanasheria kubaini kiini cha tatizo hilo,” alisema Msopa.
Hata hivyo, akizungumza jana jioni, Mkurugenzi wa
Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema kuwa viongozi hao wa dini
mara zote walipoomba kukutana na viongozi wa serikali, akiwemo Rais,
hawakupitia kwa mtu yeyote isipokuwa waliomba moja kwa moja na
wakakubaliwa.
“Hivyo, hawana sababu ya kupitia kwa watu wengine kuomba kukutana na viongozi wa serikali,” alisema.
Salva aliongeza kuwa mgomo wa madaktari umeisha na walioamua kuendelea
na kazi hii muhimu sana ya kutibu binadamu wamerudi kazini, jambo
ambalo ni jema sana.
Alisema kuwa sasa si wakati wa kulumbana tena bali ni wakati wa
kusonga mbele badala ya kurudi nyuma kwa sababu hakuna mgomo tena wa
kujadiliwa.
“Tangu madaktari walipoanza kudai maslahi zaidi, serikali ilifanya
jitihada kubwa za kukutana nao. Mbali na Kamati ya Majadiliano ya
Serikali, madaktari pia wamekutana na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, kamwe serikali haijapata kukataa kukutana na viongozi wa
madaktari,” aliongeza Salva.
Alifafanua kuwa mara ya mwisho madaktari hao walipoitwa kukutana na
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, walikataa wakidai
kuwa waziri hakuwa na jambo jipya la kuwaambia.
Katika tamko lao hilo, pia viongozi hao pamoja na kudai tume huru
waliomba serikali kufuta kesi iliyofunguliwa dhidi ya madaktari
waliofukuzwa kutokana na mgomo na kuwarejesha kazini ili kumaliza
mgomo huo waliodai unaathiri afya za Watanzania.
Kuhusu afya ya Dk. Ulimboka anayeendelea na matibabu katika hospitali
moja nchini Afrika Kusini, mmoja wa wanafamilia hiyo ambaye hakupenda
jina lake liandikwe gazetini, alisema anapata nafuu.
Hata hivyo, ndugu huyo ambaye hakupenda kuzungumza kwa kirefu
alionyesha kukerwa na taarifa za vyombo vya habari vinavyoripoti afya ya
Dk. Ulimboka kuwa ni mbaya sana, akisema kuwa si kweli

Post a Comment