TFF: Simba, Yanga, Azam wekeni heshima Cecafa

SHIRIKISHO la Soka Tanzania(TFF), limeziasa klabu za Simba, Yanga na Azam kutumia vema uwenyeji wao kulibakisha Kombe la Kagame ili kulinda heshima katika michuano hiyo mikubwa Afrika Mashariki na Kati.

Michuano hiyo ambayo imepangwa kuanza mwishoni mwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa Taifa na ule wa Chamazi na itashirikisha timu 10 kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Cecafa.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema jana kuwa hii ni nafasi nyingine kwa timu za Tanzania kuendeleza heshima yake kwa kutumia vyema uwenyeji wake katika kutwaa kwa Kombe la Kagame.

Alisema kwa upande wa maandalizi, kila kitu kinakwenda vizuri na wanaendelea kuwasiliana na viongozi wa ngazi za juu ambao ni Cecafa katika kupanga jinsi ya timu zitakapofikia kwa maana ya malazi na chakula na ratiba nzima ya mazoezi na kupangiwa viwanja watakavyotumia.

"Kikubwa ninachoweza kusema kwa sasa ni kuzitakia timu za Tanzania zitakazotuwakilisha zitambue uwenyeji wao ni chachu ya kuhakikisha wanatumia vema kulinda heshima kwa kulibakiza kombe hilo," alisema Angetile.

Aliongeza kuwa maandalizi kwa ujumla yanakwenda vizuri na wameendelea kuwasiliana na wahusika wakuu ambao ni Cacafa kupanga utaratibu pindi timu zitakapowasili kuanzia keshokutwa Alhamisi, wapi zitafikia na kufahamu utaratibu mzima wa viwanja vya mazoezi.

Timu nyingine zitakazoshiriki ni pamoja na APR (Rwanda), URA (Uganda), Atletico (Burundi), Ports (Djibouti), Wau Salaam (Sudan ya Kusini), na Vital Club ya DR Congo.

Post a Comment

Previous Post Next Post