KAMBI ya upinzani bungeni imeeleza kutilia shaka uteuzi wa Rais
Jakaya Kikwete kwa nafasi mbalimbali zikiwemo za ukuu wa wilaya, ikidai
kuwa wateule wengine ni kama wamelipwa fadhila za kisiasa.
Akisoma maoni ya kambi hiyo kwa Wizara ya Katiba na Sheria, mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema uteuzi huo umekuwa ukichangia
kudidimia kwa ufanisi wa kazi kwenye maeneo mbalimbali.
Aliongeza kuwa wakuu wa mikoa na wilaya ni makada wa CCM na
wanatekeleza majukumu yao kwa kulinda maslahi ya chama hicho tawala
wakati Tanzania inafuata mfumo wa vyama vingi.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Rais Kikwete alitumia
mamlaka yake chini ya ibara ya 2(2) ya Katiba kugawa mikoa mipya ambayo
wakuu wake ni makada wa CCM.
“Wakuu wa wilaya wamekuwa ni wajumbe wa vikao vyote vikuu vya CCM
katika ngazi ya Wilaya, Katiba ya CCM Toleo la 1982, Mkuu wa Wilaya ni
mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya (ibara ya 42(3); ni mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Wilaya (ibara ya 44(3); na ni mjumbe wa Kamati ya
Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya (ibara ya 46(3),” alisema.
Lissu alisema kuna ushahidi wa kutosha kwamba kugawa mikoa na wilaya
ni namna tu ya kupata fursa ya kuwapatia makada wa CCM ambao kwa sababu
mbalimbali wamekosa nyadhifa na marupurupu serikalini kwa kuwateua kuwa
wakuu wa mikoa na wa wilaya.
“Uteuzi wa wakuu wapya wa mikoa na wilaya uliofanywa katika siku za
karibuni na Rais Kikwete, kati ya wateuele wake wakuu wa mikoa wapya,
wawili ni wabunge wa Viti Maalum katika Bunge hili hili, kati ya wakuu
wapya wa wilaya, watano ni wabunge wa Viti Maalum katika Bunge hili
hili; 15 ni waliowahi kuwa wabunge au wabunge wa Bunge la Afrika
Mashariki na 22 waligombea ubunge lakini wakashindwa kwenye hatua za
kura za maoni za ndani CCM au kwenye Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa kuna utata mkubwa wa kikatiba kuhusiana na baadhi
ya wateuliwa wa ukuu wa mikoa na wilaya ambapo orodha ya wakuu hao
inaonyesha kuwapo kwa wanajeshi nane, ambao kati yao watatu wanatajwa
kuwa maafisa wastaafu na waliobaki hawatajwi kama wastaafu na hiyo
inaelekea bado wako katika utumishi wa jeshi.
Aliongeza kuwa uteuzi wa baadhi ya wakuu wapya wa wilaya unaashiria
kukithiri kwa rushwa na ufisadi na kukosekana kwa maadili kwa mamlaka ya
uteuzi ambapo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Wilson Elisha
Nkhambaku, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, aliteuliwa na CHADEMA
kuwa mgombea wake wa ubunge katika Jimbo la Singida Magharibi.
Alisema mgombea huyo alirubuniwa na CCM na kuamua kujiengua CHADEMA
muda mfupi baada ya kampeni za uchaguzi kuanza rasmi na alionekana
katika mkutano wa kampeni za uchaguzi wa CCM katika Jimbo la Kibaha
Vijijini na sasa kateuliwa kuwa mkuu wa wilaya.
“Kifungu cha 48 cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343 ya Sheria za
Tanzania kinaruhusu mgombea ubunge yeyote aliyeteuliwa na Msimamizi wa
Uchaguzi kujitoa katika kugombea uchaguzi husika.
Hata hivyo, Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 91B cha Sheria hiyo
kinatamka wazi kwamba ni kosa la jinai ya rushwa ya uchaguzi kumrubuni
au kumshawishi mgombea kujitoa kugombea kwa malipo, au ahadi ya malipo.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, adhabu ya kosa hilo ni kifungo kisichozidi
miaka mitano jela,” alisema.
Aliongeza kuwa kifungu cha 21(1)(b) cha Sheria ya Gharama za
Uchaguzi, 2010 kinakataza mtu yeyote, moja kwa moja au kwa namna
nyingine yoyote, yeye mwenyewe, wakala wake au kupitia chama chake cha
siasa, kwa niaba yake kutoa au kusaidia kutoa au kumpatia wadhifa au
sehemu ya ajira mpiga kura au mtu mwingine yeyote kwa nia ya kumshawishi
mpiga kura huyo kuacha kupiga kura au kumrubuni kutenda kitendo hicho.
Lissu alisema kwa mujibu wa kifungu cha 94 cha Sheria ya Uchaguzi,
makosa haya mawili ya jinai yana adhabu ya faini isiyopungua sh laki
tano au kifungo cha kati ya mwaka mmoja hadi mitatu jela au vyote viwili
kwa pamoja.
Lissu alisema uteuzi wa Nkhambaku kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu ni
ushahidi wa wazi wa rushwa ya uchaguzi na ni wazi kiongozi huyo
alirubuniwa au kushawishiwa kujitoa kugombea ubunge kwa niaba ya
CHADEMA.
Alikwenda mbali zaidi akisema kuwa kambi yao imeshangazwa na
kusikitishwa sana na uteuzi wa Kifu Gulamhussein Kifu kuwa Mkuu wa
Wilaya ya Mbarali.
Lissu alibainisha kuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, Kifu
alichaguliwa kuwa mbunge wa Kigoma Kusini kupitia NCCR-Mageuzi lakini
matokeo ya uchaguzi wake yalipingwa katika Mahakama Kuu na Juni 18,
2002, Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika Shauri la Rufaa Na. 2 la
2002 katika Manju Salum Msambya dhidi ya Mwanasheria Mkuu na Kifu
Gulamhussein Kifu, ilifuta matokeo ya uchaguzi.
Alisema kuwa Kifu alienguliwa kwa sababu Mahakama ya Rufani
ilithibitisha kwamba mtu huyo alifanya kampeni kwa misingi ya ukabila.
Lissu alinukuu kauli hizo za ukabila zilizomtia hatiani kuwa wakati wa
kampeni za uchaguzi huo Kifu alisema: “... Waha wenzangu tuelewe kwamba
mwaka huu ni mwaka wetu kujikomboa. Tumetawaliwa na kabila la Wabembe
kwa muda mrefu. Kabila la Wabembe tunajua ni watu wa Kongo siyo wa
Tanzania.
Ni ajabu Waha tulio wengi katika jimbo hili tuendelee kutawaliwa na
kabila chache. Muha popote alipo ahakikishe anipigie mimi Muha mwenzie.
Angalieni wanakuja watu huku. Yuko mtu aliyepandikizwa na Msambya. Huyu
mtu anakuja na Kabourou.... Kabourou na Msambya wote ni damu ya Kongo,
wote ni Wanyakumawe,” alisema Lissu.
Katika mkutano mwingine wa kampeni, Mahakama ya Rufani ilithibitisha
kwamba Kifu alitamka maneno yafuatayo: “Tumetawaliwa na wageni kwa muda
mrefu ... umefika wakati wa kujikomboa kutoka kwa wageni kutoka
Kongo.... Ni wakati mzuri kunichagua mimi kama Muha, Muha mwenzenu ...
kwa kuwa sisi ndio tulio wengi katika jimbo hili,”
Lissu alihoji kuwa mtu huyo aliyepatikana na hatia ya kufanya siasa za kibaguzi za aina hii ameteuliwaje kuwa mkuu wa wilaya
إرسال تعليق