BAADA ya kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, viongozi wa vyama vya
madaktari wamedai maisha yao yako hatari hali iliyowalazimu kuomba
ulinzi Umoja wa Mataifa na makundi mbalimbali ya kutetea haki za
binadamu.
Madaktari hao wamesema hawana imani na maofisa wa serikali ya Rais
Jakaya Kikwete, wanaotishia usalama wa maisha yao kwa namna tofauti hasa
baada ya tukio la Dk. Ulimboka la Juni 27 mwaka huu.
Barua ya madaktari hao kwenda kwa Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa
hapa nchini ya Julai 7, 2012, madaktari wameeleza namna maofisa wa
serikali wanavyotishia usalama wa maisha yao hao na kuwaeleza namna
walivyowatuma wenzao Afrika Kusini kuhakikisha Dk. Ulimboka anapoteza
maisha.
Pia barua hiyo yenye kumb. Na.MAT/UN/SU/01, imetumwa kwa Mwenyekiti wa
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Namala Mkopi, Shirika la Human
Rights Watch na Amnesty International.
Taasisi nyingine zilizopelekewa nakala ya barua hiyo ambayo Tanzania
Daima ina nakala yake ni Kituo cha Haki za Binaadam (LHRC), SIKIKA
Tanzania, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake (TAMWA).
“Hata hivyo, watu kutoka serikalini waliihakikishia MAT kwamba timu ya
wasaidizi wao imeenda Afrika Kusini kuhakikisha Dk. Ulimboka anarudi
nyumbani akiwa maiti.
“Kwa kuongezea hapo, viongozi wa MAT tunapokea vitisho kwa njia ya
ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu na wakati mwingine tunapigiwa simu
na namba zisizopatikana tukitishiwa maisha,” ilieleza sehemu ya barua
hiyo iliyosainiwa na Dk. Mkopi.
Aidha, barua hiyo imeuomba Umoja wa Mataifa kuwahakikishia madaktari
usalama wa Dk. Ulimboka kwenye hospitali anayotibiwa na kuwalinda
madaktari wengine hasa viongozi wa vyama na jumuiya ya madaktari.
Kadhalika barua hiyo imeuomba umoja huo kuushauri mfumo wa sheria za
Tanzania kutokubali kutumika kwa faida za kisiasa na kulitaka Bunge
kubaki na majukumu yake ya Kikatiba ya kuiwajibisha serikali kwa vifo
vya watu kama matokeo ya mgomo unaoendelea.
Katika barua hiyo madaktari hao wameeleza namna Dk. Ulimboka
alivyoteswa na watekaji hao kwa kung’olewa kucha, meno na kuumizwa
sehemu mbalimbali za mwili wake huku akimtambua ACP Msangi kuwa miongoni
mwa watekaji hao.
Walieleza namna polisi wa kituo cha Bunju walivyoshindwa kuwapa
ushirikiano kwa haraka ili kumuwahisha majeruhi huyo kwenye Hospitali ya
Taifa Muhimbili na jinsi walivyokuwa wakizuiwa na magari ya askari kwa
lengo la kumchelewesha asipate huduma za kitabibu.
“Akiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi Kitengo cha Mifupa
Muhimbili (MOI), Dk. Ulimboka licha ya maumivu makali aliyokuwa nayo
alimtambua ACP Msangi kuwa ni miongoni mwa waliomteka na kumtesa,”
ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kubainisha kwamba ACP Msangi ni
kiongozi wa tume iliyoundwa kuchunguza suala hilo.
Ikulu yasononesha viongozi wa dini
Baadhi ya viongozi wa dini waliojitolea kusuluhisha mgogoro baina ya
madaktari na serikali, wameeleza kusononeshwa na jibu la Ikulu la
kukataa kuonana nao huku wakibainisha kwamba jukumu lao kubwa ni
kuhakikisha amani inatawala.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi hao, Msemaji wa Kamati ya Vijana wa
Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata), Said Mwaipopo, alisema licha ya jibu
hilo wanaendeleza juhudi za kuhakikisha mgogoro huo unamalizika kwa njia
za amani.
“Hatukatishwi tamaa na jibu la Ikulu kazi yetu kubwa ni kuhakikisha
amani inakuwepo… ndiyo maana jana tulikutana na viongozi wa madaktari
tukawaeleza kwamba njia bora ya kufanya ni kuandika barua na kuieleza
jamii kupitia vyombo vya habari kwamba wanaomba msamaha kwa Rais,
wananchi na serikali.
“Kitu kinachotusikitisha vijana wale walikataa ushauri wetu tukagundua
kwamba inawezekana nyuma yao kuna siasa zinaingia,” alisema Mwaipopo.
Akijibu suala hilo Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Edwin Chitage,
alikiri kukutana na viongozi hao jana na kueleza kwamba walichokubaliana
ni kusubiri barua rasmi kutoka Ikulu ikiwataka madaktari hao kuandika
barua kuomba msamaha kwa Rais, Watanzania na serikali.
“Ni kweli lakini alichokisema Mwaipopo ni kwamba alipigiwa simu na
watu waliodai kwamba wako Ikulu, hivyo wakawaambia viongozi hao wa dini
watuambie madaktari tuandike barua ya kuomba msamaha.Tunaomba msamaha
kwa nini,” alihoji.
Dk. Mkopi aliongeza kuwa madai yao hayajatekelezwa licha ya kuwepo kwa
muda mrefu tangu mwaka 2005 na kwamba kama serikali haina dhamira ya
kweli ya kumaliza mgogoro huo utaendelea hata baada ya miaka 10.
Kukutana na Dk. Mwinyi
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk. Godbless Chale alisema
walipokea simu kutoka kwa Waziri mpya ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk.
Hussein Mwinyi ikiwataka kwenda kumweleza sababu za mgomo wao.
“Kweli Dk. Mwinyi alitupigia simu akatuita alisema hajui madai yetu
hivyo twende tukamweleze hivi kwa akili ya kawaida kweli ofisi inakosa
nyaraka za kumbukumbu?!! Tunaona hayupo ‘serious’.
“Kabla hajatuita wizara yake iliteua wajumbe watatu Naibu Katibu Mkuu,
Naibu Mganga Mkuu Dk. Donald Mbando na Mkurugenzi wa Rasilimali
tukaketi nao kuwaeleza siku chache baadaye waziri anasema hajui madai
yetu hii tumeona ni ‘kamchezo’ wanataka kutufanyia,” alisema Dk.
Godbless
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz

إرسال تعليق