Madaktari wasitisha maandamano
CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimesitisha maandamano ya
amani yaliyokuwa yafanyike kesho na badala yake wataendelea kuomba
kibali kwa ajili ya wiki ijayo.
Madaktari hao juzi walitoa tamko la kufanya maandamano makubwa ya
amani jijini Dar es Salaam ili kupinga dhuluma na uonevu dhidi ya
taaluma muhimu ya udaktari na madaktari wenyewe.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili jana jijini Dar es Salaam,
Katibu wa MAT, Dk. Rodrick Kabangila, alisema pamoja na hatua ya Jeshi
la Polisi kuyapiga marufuku maandamano hayo bado wataendelea kuomba
kibali kwa siku zijazo kwani ni haki ya raia.
Alidai kuwa sababu zilizotolewa na jeshi hilo ni za kisiasa kwa kuwa
hoja zilizotolewa na wanataaluma hao hazina uhusiano na mgomo
unaoendelea nchini.
“Hatuwezi kuandamana maana wanaweza kutudhalilisha na makoti yetu
meupe ingawa jeshi hilo limetumika kisiasa …sisi tutaendelea kupigania
haki zetu kwa kuomba tupewe kibali kwa siku zijazo za wiki ijayo,”
alisema.
Katibu huyo alisema kuwa jeshi hilo halina sababu ya kuhofu vurugu
kuibuka katika maandamano hayo kwa kuwa ina vikosi vya kutosha kuweza
kukabiliana na fujo zozote.
Alisema kuwa madaktari wataendelea kupigania haki zao na kupinga
unyanyasaji wanaofanyiwa na serikali likiwemo suala la kutekwa na
kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madakatri, Dk. Steven Ulimboka.
Kwa mujibu wa Dk. Kabangila, alitaja lengo la maandamano ilikuwa ni
kupinga na kusikitishwa na dhuluma inayofanyiwa taaluma hiyo kwa
kuzingatia uwiano duni wa madaktari hapa nchini ambapo daktari mmoja
hutibu wagonjwa 30,000 kwa mwaka chini ya viwango vya kimataifa.
Alisema jumla ya madaktari 400 walio chini ya usimamizi wa madaktari
bingwa, wamesitishiwa usajili wao na wengine kusimamishwa kazi bila
kujali umuhimu wao kwa mustakabali wa taifa na wananchi wake.
Dk. Kabangila alisema kuwa nyingine ni kushinikiza serikali iunde tume
huru kwa ajili ya kuchunguza suala la Dk. Ulimboka itakayofanya kazi
haraka na wahusika wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
“Maandamano hayo yalipangwa kuanzia nje ya Hospitali ya Taifa
Muhimbili, tutaishia kwenye geti la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
tukiwa na mabango ya kulaani kitendo cha kutekwa, kupigwa na kutelekezwa
kwenye msitu wa Pande alichofanyiwa Dk. Steven Ulimboka,” alisema.
Post a Comment