WAKATI Shirika lisilo la kiserikali la SIKIKA, likidai kupokea kwa
masikitiko makubwa taarifa ya Baraza la Madaktari Tanganyika kuwafutia
leseni za kutibu madaktari wanafunzi (interns) 319 juzi na kutaka
warejeshwe mara moja, Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania (BAHAKITA),
linakusudia kuwashitaki mahakamani madaktari waliogoma.
Mkurugenzi wa SIKIKA, Irenei Kiria, alisema kuwa wanamtaka, Dk. Donan
Mmbando, ambaye anaongoza baraza hilo kwa niaba ya serikali,
kuwarejeshea leseni zao interns haraka iwezekanavyo na kuwarudisha
kwenye vituo vyao vya kazi.
Alisema kuwa namna serikali inavyoshughulikia mgogoro wa madaktari,
inaonesha wazi kuwa haina uwezo wa kutatua migogoro ya wafanyakazi wake
badala yake inatumia hujuma, vitisho na ubabe.
“Mgomo huu unaoendelea wa madaktari nchini ni wa kipekee kwa sababu
haujaitishwa na Chama cha Madaktari (MAT) na kwamba unapigania kuboresha
huduma za afya kwa wananchi,” alisema Kiria.
Alisema tangu mgomo huo uanze, serikali haijawahi kuwa na nia ya dhati
kushughulikia madai ya madaktari zaidi ya kuahirisha mazungumzo,
kudanganya umma kuhusu hatua za makubaliano kwamba imetatua matatizo ya
huduma za afya.
Kiria aliongeza kuwa pengo la madaktari nchini ni kubwa kufikia
takriban asilimia 60, hivyo si busara kuwanyanyasa wale wachache
waliokubali kufanya kazi katika mazingira hatarishi kiafya na
vitendeakazi duni au haba.
Kwamba kwa mujibu wa tafiti za SIKIKA, hospitali nyingi nchini hazina
mashine za kuchunguza maradhi na zilizopo ni mbovu kwa muda mrefu bila
jitihada za kutengeneza, mfano X-ray na CT-Scan.
“Mwenyekiti wa Baraza la Madaktari ndiye Mganga Mkuu wa wizara,
mwajiri. Hatuna taarifa kama uchunguzi wa kutosha ulifanyika kwa kila
intern ushiriki wake katika mgomo kabla ya kufutiwa leseni.
Hivyo, tunahitaji madaktari zaidi kuhudumia wananchi, uamuzi wa
kuwafukuza ni kutowajali wananchi, hasa wakati huu ambao viongozi wengi
wa serikali hutibiwa nje ya nchi,” alisema.
Hata hivyo, BAHAKITA kwa upande wao wameweka msimamo wa kwenda
mahakamani kuwshitaki madaktari waliogoma iwapo litabaini kuwapo kwa
vifo vya watu vilivyotokana na mgomo huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu
wa Baraza hilo, Said Mwaipopo, alisema wamekusudia kufanya hivyo baada
ya kuona kwamba madaktari hawataki suluhu wala kusikiliza ushauri wao.
Mwishoni mwa juma lililopita, Mwaipopo akiwa na baadhi ya viongozi wa
madaktari walioko kwenye mgomo, alinukunuliwa na vyombo mbalimbali vya
habari akimwomba Rais Jakaya Kikwete akutane nao ili kuzungumzia suala
la madaktari ombi lililokataliwa na Ikulu kwa maelezo kwamba hakuna
mgomo tena.
Hata hivyo baada ya Ikulu kukataa ombi lao Mwaipopo alizungumza na
Tanzania Daima akisema amewashauri viongozi wa madaktari kuandika barua
ya kuomba msamaha kwa wananchi, serikali na Rais Kikwete kisha kuweka
bayana suala hilo kwenye vyombo vya habari.
Katika majibu yake kuhusu suala hilo, Dk. Edwin Chitage, ambaye ni
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, alikiri kukutana na Mwaipopo akiwa na
viongozi wengine na kusema haoni sababu ya kuomba radhi kwa vile kudai
masilahi na mazingira bora ya kazi si kosa.
“Wapo wanaosema mgogoro umeisha lakini ukweli si huo, mgogoro bado upo
na huu ulianza mwaka 2005 bila dhamira ya dhati ya kutafuta suluhu,
utaendelea hata baada ya miaka 10, naomba jamii ielewe hatulazimishi
kukutana na mtu muhimu hapa ni dhamira ya dhati kwanza,” alisema.
Lakini katika tamko lao, Mwaipopo aliweka bayana kwamba lengo la
kuwaburuza mahakamani madaktari hao ni barua waliyoandika kwa Umoja wa
Mataifa (UN) wakiomba ulinzi huku akisisitiza kwamba kitendo hicho ni
kuudhalilisha utawala wa Rais Kikwete.
Kuhusu madaktari wanafunzi kunyang’anywa leseni zao, Dk. Chitage alisema hawashtushwi na jambo hilo kwa kuwa walilitegemea.
Afya ya Dk. Ulimboka
Akizungumzia hali ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk.
Steven Ulimboka, ambaye baada ya kutekwa, alipigwa na kutelekezwa kwenye
msitu wa Pande nje ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Chitage alisema
anaendelea vizuri.
Dk. Ulimboka aneendelea na matibabu nchini Afrika Kusini. Na Dk.
Chitage alisema wanamshukuru Mungu kwamba mwenyekiti wao anaendelea
vizuri kila siku afya yake inazidi kuimarika na hata anapozungumza naye
kwenye simu anamsikia kwamba amepata nafuu sana

Post a Comment