KAMBI ya upinzani bungeni imeitaka serikali kuyarejesha mashamba
yaliyoshindwa kuendelezwa na wawekezaji na yagawiwe kwa wananchi wenye
kuyahitaji.
Miongoni mwa wawekezaji hao ni Chavda Group, aliyeuziwa mashamba saba
yenye ukubwa wa hekta 25,000, katika maeneo tofauti hapa nchini,
ambapo mwaka 1993 alizitumia hati zake kujipatia mkopo wa dola milioni
tatu.
Kauli hiyo imetolewa jana bungeni na Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, alipokuwa akitoa hotuba ya
kambi yake kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2012/2013.
Mdee alisema familia ya Chavda iliahidi kufufua mashamba ya mkonge
Tanga ndani ya miaka 10, na kupata dola milioni 42 lakini walipopata
fedha hizo hawakufanya lolote kwenye mashamba hayo na hakuna hatua
zilizochukuliwa dhidi yao.
”Tuwachukulie wawekezaji wa aina hii kama ni ’waporaji’ na hawana
tofauti na majambazi wanaoiba benki kwa kutumia nguvu,” alisema Mdee.
Aliongeza kuwa wanaitaka serikali kuyarejesha serikalini bure pasi na
fidia mashamba hayo kwa ajili ya kutafuta wawekezaji wengine wenye
mtaji wa kutosha watakaoyaendeleza.
Alibainisha kuwa mashamba ambayo tayari yana wakulima wadogo wadogo
wanaoendesha shughuli zao za kilimo, serikali ipange utaratibu wa
kuwamilikisha wananchi maeneo husika
ili kuondokana na ile dhana ya ’uvamizi’ au kukodishwa ardhi kwa ajili
ya kilimo. Zoezi hili lazima lifanywe kwa uwazi ili kuepuka udanganyifu
uliotokea katika maeneo mengine ya nchi ambapo vigogo na watu wenye
nafasi zao walijitwalia ardhi wakijifanya na wao ni sehemu ya
wanakijiji!
Kampuni ya uwindaji yatafuta madini
Kambi hiyo imesema Tanzania imegeuzwa shamba la bibi na kikundi cha
mafisadi ambapo imeshuhudia mkataba ilioingiwa baina ya kampuni za
Uranium Resourses PLC, Western Metals Limited na Game Frontiers of
Tanzania Limited.
Mkataba ambao umetengenezwa na Kampuni ya Kitanzania ya REX ATTORNEYS
Machi 23, 2007, unaihusu kampuni ya uwindaji, inayofahamika kwa jina la
Game Frontiers of Tanzania Limited inayomilikiwa na Mohsin M.
Abdallah na Nargis M. Abdallah.
Mdee alisema kampuni hiyo ya uwindaji, imeingia mkataba na kampuni
mbili za kigeni, za kufanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya uranium
katika Kijiji cha Mbarang’andu.
Alisema sheria za uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 1974 (Sheria ya
zamani) na Sheria mpya The wildlife Conservation Act, Act no 5 of 2009.
Sheria hizi zinamruhusu mtu aliye na leseni ya uwindaji, kuwinda wanyama
tu.
Aliongeza kuwa kambi hiyo inaitaka serikali ilieleze Bunge uhalali wa
mkataba kati ya Game Frontiers na Uranium Resourses PLC na Western
Metals.
Mapema akiwasilisha bajeti yake, Waziri wa Ardhi, Profesa Anna
Tibaijuka, alisema kuwa wanatarajia kutumia sh bilioni 60 kutoka katika
bajeti yao sh bilioni 101.7 ilizoziomba mwaka 2012/2013 kuendeleza mji
mpya wa Kigamboni.
Profesa Tibaijuka alisema mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni
utahitaji sh trilioni 11.6 mpaka kukamilika kwake na serikali imejipanga
kutafuta kiasi hicho cha fedha.
Alisema sh bilioni 60 walizotenga kwa mwaka 2012/2013 ni sawa na
asilimia 10 ya fedha zote zinazohitajika katika mradi huo na sh bilioni
605 serikali itatumia mbinu za kisasa kuzitafuta.
Aliziagiza halmashauri za wilaya zote nchini kusimamia ipasavyo
masuala ya ardhi kwa kufuata sheria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
wananchi wanaokaidi mipango miji, wanaovamia maeneo ya wazi na kujenga
kwenye fukwe hawalipwi fidia.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz

إرسال تعليق