Serikali yatakiwa kuweka wazi nyongeza ya mishahara

0digg
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Komban
MBUNGE wa Kasulu Mjini, (NCCR - Mageuzi) Moses Machali amesema Serikali inatakiwa iweke wazi nyongeza ya mishahara katika mwaka wa fedha 2012/13.

Alisema hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, haikuweka wazi ni kiasi gani cha mshahara kilichoongezeka katika kada mbalimbali hapa nchini.

“Serikali iseme kila kada imeongezewa kiasi gani. Mnasema mtaongeza mshahara kutokana na bajeti itakavyokuwa kwa nini msiseme hiyo bajeti itakavyowaruhusu mtaongeza kiasi gani?” alisema Machali.

Aidha, Machali aliishutumu Serikali kwa kushindwa kutumia maoni au tafiti zinazofanywa na tume mbalimbali zinazoundwa na Serikali.

Alisema, tume zinatumia fedha nyingi na iwapo tafiti au matokeo yake hayatumiwi na Serikali hayo ni matumizi mabaya ya fedha.

“Nakumbuka iliundwa tume ya Ntukamazina kufanya utafiti kuhusu namna ya kuboresha mslahi ya watumishi wa Serikali, lakini mpaka sasa utafiti wa tume hiyo haujawekwa wazi. Ina maana tafiti hizo zinawekwa katika makaratasi tu?” alisema.

 

Machali alizungumzia pia suala la baadhi ya wakurugenzi kutokuhakiki madai ya walimu kwa umakini na kusababisha baadhi ya walimu hao kukosa haki zao.

Alisema kuwa, wapo walimu wanaodai fedha za likizo, uhamisho na za masomo, lakini wanazikosa kwa kuwa madai yao hayahakikiwi ipasavyo.

“Hili jambo linasababisha watumishi wa Serikali kukosa haki zao. Kwa nini watumishi wa Serikali wanachezewa kama kichaka cha mwendawazimu?” alihoji Machali.
Chanzo:- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post