FERGUSON AMFAGILIA PATRICE EVRA, AKISAJILI MRITHI

FERGUSON AMFAGILIA PATRICE EVRA, AKISAJILI MRITHI

MANCHESTER, England

KOCHA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amemsifu beki wake Patrice Evra akimuita “askari kamili” – kauli aliyoitoa huku usajili wake wa karibuni wa kinda Alexander Buttner ukitafsiriwa na wengi kama mrithi wake Old Trafford.

Evra, Mfaransa mahiri katika beki ya kushoto, amekuwa tegemeo la Mashetani Wekundu kwa miaka sita ya uwepo wake klabuni hapo, lakini Fergie juzi alimuonya beki wake mpya aliyemgharimu pauni milioni 4, Buttner, kujipanga katika nafasi hiyo.

Bosi huyo wa United alisema: “Tulichofanya ni kulinda matarajio yetu ya baadaye. Hiyo ndiyo busara. Evra ana miaka 31 na Alex amekuja hapa kutoa changamoto katika nafasi yake.

“Lakini ikumbukwe pia kwamba hakuna mchezaji aliyecheza mechi nyingi kuliko Evra katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Amefanya hivyo hata katika mazingira magumu ikiwamo kuwa na majeraha.

“Amekuwa mhimili wetu katika ulinzi akipanda na kushuka kwa miaka mitano. Ni jumla ya mechi 240 alizocheza kipindi hicho, zinazomfanya sasa Patrice kuwa askari kamili.”

Tangu uhamisho wake wa pauni milioni 5.5 akitokea Monaco ya Ufaransa miaka sita iliyopita, Evra amecheza jumla ya mechi 291 akiwa na United, akitwaa kila taji na kujiwekea historia na heshima kubwa katika soka la England.

Lakini sasa Fergie yuko tayari kuanza kumbadilisha kwa kumtumia Buttner, 23, Mholanzi aliyejiunga United akitokea Vitesse Arnhem, akifuata nyayo za nyota wengine waliotua hapo kiangazi hiki, kina Shinji Kagawa, Nick Powell, Angelo Henriquez na Robin van Persie.

Ferguson alimuelezea nyota huyo kwa kusema: “Tumemfuatilia kwa muda mrefu sana Alex. Ni mlinzi mahiri aliye na uwezo wa kuanzisha mashambulizi ya kutokea nyuma na kurejea haraka kwenye nafasi yake ya ulinzi. Tunatarajia atakuwa hivyo akiwa nasi.”

Post a Comment

Previous Post Next Post