MASCHERANO AMTETEA MLINDA MLANGO BARCELONA

MASCHERANO AMTETEA MLINDA MLANGO BARCELONA

BARCELONA, Hispania

KIUNGO Javier Mascherano, amemtetea Victor Valdes, baada ya mlinda mlango huyo wa Barcelona kuizawadia bao muhimu Real Madrid, katika ushindi wa Barca wa 3-2 wa mechi ya kuwania Super Cup kwenye Uwanja wa Nou Camp katikati ya wiki.

Valdes alishindwa kugusa vema mpira wake wa kwanza na kumruhusu winga wa Madrid, Angel Di Maria kuipa timu yake bao hilo muhimu, lakini Mascherano akasema Barca kamwe haiwezi kuacha aina yake ya soka.

Akaongeza kuwa, kuuchezea mpira ni kati ya falsafa za Barca, na Valdes anabaki kuwa mtu muhimu wa kuigwa Nou Camp.

“Ilikuwa aina ya uchezaji ambayo ni kipa wa Barca tu anayeweza kucheza, hiyo ni aina ya uchezaji ya klabu hii na klabu inalitambua hilo,” alisema Mascherano kuviambia vyombo vya habari kuelekea pambano la La Liga dhidi ya Osasuna.

“Tunapendelea kufanya makosa yasiyo ya kawaida (kama alilofanya Valdes), ili kuendelea kubaki kama tulivyo.”

Katika hatua nyingine, beki wa pembeni wa Barca, Mfaransa Eric Abidal, ameanza mazoezi ya gym kwa mara ya kwanza, tangu alipofanyiwa upandikizaji wa ini, Aprili mwaka huu.

“Nimeanza rasmi mazoezi ya ndani, kwa muda mfupi tu kwa sasa,” alisema Abidal juzi.

Beki huyo awali alitarajiwa kurudi tena dimbani Desemba mwaka huu, kama alivyoandika kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook

Post a Comment

Previous Post Next Post