Haya, Simba yamchukulia 'RB' Twite Kumkamata uwanja wa ndege

Simba yamchukulia 'RB' Twite Kumkamata uwanja wa ndege
*
Michael Momburi,Arusha
SAKATA la beki Mbuyu Twite limechukua sura mpya baada ya uongozi wa Simba kudai umemchukulia RB ya Polisi beki huyo kwa lengo la kumkanata dakika yoyote atakayotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere akitokea Rwanda.
Twite alisaini mkataba na Simba jijini Kigali hivi karibuni kabla ya kubadili uamuzi na kusaini tena Yanga na kurejesha fedha za Simba ingawa waligoma kuzipokea wakimtaka aje mwenyewe.
Uongozi wa Simba umesema haumtaki mchezaji huyo, lakini unataka arejeshe kwa mkono wake fedha alizochukua dola 32,000 na aeleze kwa nini aliwatapeli.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' aliiambia Mwananchi jana kuwa lazima wamkamate mchezaji huyo kwa madai kuwa ni tapeli.
Hakuna sheria yoyote ambayo inamlinda mhalifu hata kama ni raia wa kigeni, sisi hatujapeleka jina lake TFF kwa vile tumeamua kuachana naye, lakini tunataka arudishe fedha zetu na atuambie kwa nini alitutapeli.
Sisi tumeshamchukulia RB na tutamkamata palepale uhamiaji Uwanja wa Ndege, akitua tu tunae mpaka kieleweke, hatuwezi kukubali kutapeliwa.
Sisi kuna watu walituletea zile fedha zake, lakini tukakataa hatukupokea mpaka alete mwenyewe. Tunataka pia mamlaka husika zifanye kazi na afungiwe kwa kufanya ubabaishaji na kusaini mikataba miwili,alisisitiza Kaburu.
Wakati huo huo; Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic amesisitiza kuwa kambi ya Arusha imebadilisha kwa haraka timu yake na kusisitiza kuwa imeiva kila idara tayari kwa Ligi Kuu ya Bara.
Mserbia huyo ambaye timu yake itacheza mechi ya ngao ya hisani dhidi ya Azam Septemba 8, amesifia kambi ya Arusha na kudai kuwa italeta mabadiliko makubwa kwa wachezaji wake.
Tuko vizuri kimazoezi na tayari kwa kushiriki michuano yoyote ile inayokuja mbele yetu, tumefanya mazoezi ya pamoja muda mrefu sasa.
Nimepata nafasi ya kuona uwezo binafsi wa kila mchezaji na jinsi gani kila mchezaji anaweza kuingia kwenye mfumo wangu, hii kambi hapa Arusha imenisaidia sana kubadili timu na kunipa faida mimi kama Mwalimu.
Wachezaji wamekuwa na nguvu sana kutokana na hii hali ya hewa ya baridi, wakirudi sehemu kama Dar es Salaam watakuwa na nguvu sana na kiwango kitapanda kwa vile hali ya hewa ya kule wameizoea.
Naamini watacheza soka la tofauti sana na ambalo mashabiki wanajua, nategemea mabadiliko mengi sana kwa vile hata aina ya wachezaji niliosajili ni wa tofauti sana na wale waliokuwapo, hii ni timu ya ushindi,alisisitiza kocha huyo kwa kujiamini huku akivuta sigara yake. Chanzo:-

Post a Comment

Previous Post Next Post