NAHODHA wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, Juma Kaseja na
Ofisa Habari, Ezekiel Kamwaga, juzi walikumbana na wakati mgumu kutoka
kwa mashabiki, mara baada ya kumalizika kwa mechi yao ya kirafiki dhidi
ya Nairobi City Stars.
Mechi hiyo maalumu kuadhimisha siku ya Simba, ‘Simba Day’ ilipigwa
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambako Wekundu wa Msimbazi,
walikubali kichapo cha mabao 3-1.
Mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, wanachama na baadhi ya
mashabiki, walimweka kati Kaseja huku wakitaka maelezo ya kina kwanini
wamelala 3-1 katika mchezo huo, wakati wao walikuwa wakihitaji furaha
katika sherehe hizo.
“Kaseja unaweza kutueleza kwa nini mmeharibu siku yetu ya Simba Day
kwa kufungwa mabao yote haya na kutupotezea pozi zote,” alihoji mmoja wa
mashabiki ambao walimzonga.
Kaseja, alilazimika kuwajibu mashabiki hao, ambao walionekana kuwa na
jazba ya kutibuliwa siku yao ya furaha ambayo iligeuka kuwa majonzi.
“Jamani nyie ni wadau na mashabiki wetu ambao ni moja ya sapoti kubwa
kwetu, kufungwa katika mchezo huu kusiwanyime raha na amani, kwani Kocha
Mkuu Milovan Cirkovic anajua nini alichokuwa akikihitaji katika mechi
hiyo na ndio maana alitutoa karibu wote kipindi cha pili wakaingia
wengine,” alijitetea Kaseja.
Mara baada ya majibu ya Kaseja, mashabiki hao walionekana kuridhika na
kumruhusu kuondoka, kabla hajatokea Kamwaga ‘Mr. Liverpool’ ambako
kibao kikamgeukia na kuwekwa kati huku wakimuhoji maswali kadhaa.
Post a Comment