NBS YATOA TAARIFA YA HALI YA UCHUMI NCHINI.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Bw. Morrice Oyuke akiongea na waandishi wa habari leo jijini
Dar es Salaam kuelezea hali ya Ukuaji wa Pato la Taifa kwa 7.1% katika
kipindi cha robo mwaka 2012.
Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) imetoa taarifa ya hali ya uchumi nchini na kufafanua kuwa
pato la taifa la Tanzania limekua kwa asilimia 7.1 katika kipindi cha
robo ya mwaka 2012 ikilinganishwa na asilimia 6.1 za mwaka jana.
Ukuaji
huo wa asilimia 7.1 unatokana na ongezeko la uzalishaji katika shughuli
mbalimbali za kiuchumi zikiwemo za kilimo, Uvuvi, Viwanda, Ujenzi na
zile za utoaji wa huduma mbalimbali za jamii.
Akitoa
taarifa hiyo jana jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa lengo la
utoaji wa taarifa hizo kwa vipindi vifupi vya vya robo mwaka unalenga
kuwapatia wadau wa Takwimu za Pato la Taifa uwezo wa kutathmini
mabadiliko ya ukuaji wa uchumi nchini.
Amesema
kuwa jumla ya thamani ya pato la Taifa katika kipindi cha robo ya mwaka
2012 ni shilingi 4,220,535 milioni ikilinganishwa na kiasi cha shilingi
milioni 3,940,261 za mwaka 2011.
Amefafanua
kuwa ukuaji wa shughuli uzalishaji katika shughuli za kilimo nchini
ulifikia asilimia 1.4 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2012
zikilinganishwa na asilimia 1.2 katika kipindi hicho kwa mwaka 2011
kutokana na upatikanaji wa mvua za kutosha nchini katika mikoa
inayozalisha mazao kwa wingi.
Amesema ukuaji katika shughuli za uvuvi ulikua asilimia
2.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2012 huku shughuli za uchumi katika
sekta ya viwanda na Ujenzi ambayo inahusisha uchimbaji wa madini na
kokoto ikikua kwa asilimia 14.3 ikilinganishwa na 0.8% za mwaka 2011.
Bw. Oyuke ameongeza kuwa ongezeko hilo la
uzalishaji wa madini ya dhahabu linatokana na uzalishaji wa wa madini
ya dhahabu kutoka kilo 8,140 kwa mwaka 2011 hadi kufikia kilo 16,736 kwa
mwaka 2012.
Pia
amebainisha kuwa shughuli za utoaji wa huduma za biashara za jumla na
rejareja, ukarabati wa magari na pikipiki na vifaa vingine vya majumbani
katika kipindi hicho zilifikia asilimia 9.0 huku shughuli za
upangishaji nyumba na biashara zikiwa 8.2 %, uchukuzi na mawasiliano
16.4%, hoteli na migahawa 3.8%, Benki asilimia 15 shughuli za uendeshaji
serikali 6.4%, Elimu 6.1% na utoaji wa huduma za Afya nchini zikikua kwa kasi ya asilimia 5.1.
Habari/Picha na Aron Msigwa - MAELEZO.
Dar es salaam.
إرسال تعليق