NYOTA YA T. ULIMWENGU YAANZA KUNG'ARA MAZEMBE

NYOTA YA T. ULIMWENGU YAANZA KUNG'ARA MAZEMBE

Ulimwengu


MAMBO yameanza kumnyookea mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu baada ya kuingizwa rasmi kwenye kikosi cha kwanza cha klabu yake, Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ulimwengu alikuwa kwenye benchi kwa dakika zote 90 jana wakati Mazembe, ikiifunga  Zamalek ya Misri mabao 2-1 kwenye Uwanja wa chuo cha Jeshi, Al-Qahirah mjini Cairo, katika mchezo ambao, Mtanzania mwenzake, Mbwana Ally Samatta ‘Sama Goal’ alifunga bao la ushindi dakika ya 44, akiunganisha pasi ya Tressor Mputu Mabi.
Uli alisajiliwa msimu uliopita Mazembe, lakini kwa muda wote amekuwa kwenye kikosi cha wachezaji wa akiba hadi hapo jana, alipokaa kwenye benchi kwa mara ya kwanza pamoja na kocha Msenegali, Lamine N’Diaye.
Katika mchezo huo wa Kundi B, Himoonde alitangulia kuifungia Mazembe inayofundishwa na Lamine N'Diaye dakika ya 34 pasi ya Mputu, lakini Omotoyossi akaisawazishia Zamalek inayofundishwa na kocha Jorvan Vieira dakika ya 36, pasi ya Mohamed Ibrahim.
Ushindi huo wa kwanza ugenini kwa Mazembe katika hatua ya makundi, unaifanya Mazembe ifikishe pointi saba, baada ya kucheza mechi nne, kushinda mbili, sare moja na Berekum Chelsea na kufungwa moja na Al Ahly ugenini.
Al Ahly iliyotoa sare ya 1-1 na Berekum Chelsea nchini Ghana leo, bado inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10, wakati wababe wapya wa Ghana wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao tano na Zamalek wanashika mkia wakiwa hawana pointi hata moja. 
Miezi miwili iliyopita, http://bongostaz.blogspot.com/ ilifanya mahojiano na Makamu wa Rais wa Mazembe, Mohamed Kamwanya kuhusu kuchelewa kwa Samatta kuingizwa kwenye kikosi cha kwanza, ambaye alisema kwamba mshambuliaji huyo anachelewa kwa sababu kiwango chake bado kidogo.
Alisema kwamba, Ulimwengu kila anapopewa ruhusa ya kurejea Tanzania kujiunga na timu za taifa, kwanza huchelewa kurudi Lubumbashi na pia hurudi akiwa hayuko fiti.
“Hicho ndio kinamchelewesha, lakini kama siyo hivyo angekuwa anacheza tu kama mwenzake. Na nyinyi watu wa vyombo vya habari mtusaidie, kwa sababu wachezaji wakija huko wanafanya anasa, wanarudi huku hawako fiti, sasa inakuwa mbaya,”alisema Kamwanya.

Post a Comment

أحدث أقدم