SIMBA AU YANGA - NGASA

MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga wamepiga hodi klabu ya Azam wakiwa na Sh20 milioni mkononi, huku mahasimu wao Simba, nao wakiwa na Sh25 milioni wakitaka kumsajili winga aliyechoka kuendelea kucheza Uwanja wa Chamazi, Mrisho Ngasa.

Uamuzi huo wa vigogo hao kumwania Ngasa, umekuja haraka kwani ni juzi tu, Azam walitoa tamko la kumruhusu nyota huyo aliyekosa namba kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Hall Stewart kuondoka kwa dau la dola 50,000.

Kupitia ukurasa wao kwenye tovuti ya facebook, Azam ilitangaza kutoa nafasi ya upendeleo kwa Yanga kwa madai kuonyesha nia ya kurudi klabu yake ya zamani.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa Azam, Patrick Kahemela alisema, ingawa dau la Simba liko juu lakini nia yao ni kumruhusu kwenda Yanga.

"Ukiangalia hapa, dau la Simba liko juu lakini sisi Azam tunawaita Yanga waje kufanya mazungumzo, pengine tunaweza kupunguza dau," alisema Kahemela.

"Kwa upande wetu tusingependa Ngasa aende Simba kwa sababu lengo letu siyo kumkomoa, nani hafahamu jinsi anavyobezwa na mashabiki wa Simba?," alisema Kahemela.

Kahemela alisema kama Yanga watashindwa, basi hawatakuwa na jinsi zaidi ya kumuuza klabu ya Simba.

"Pamoja na yote hii ni biashara, itakuwa ajabu tunaacha Sh25 milioni za Simba halafu tunachukua Sh20 milioni za Yanga," alisema Kahemela.

Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa alisema jana tayari wamekwisha wasilisha ofa yao kwa timu ya Azam FC na wanasubiri jibu kutoka kwa uongozi wa timu hiyo.

Mwesigwa alisema wanafahamu mapenzi ya Ngasa kwa Yanga kwa vile ndiyo iliyomlea mpaka kufikia kiwango cha kusajiliwa na Azam FC.

“Tumewasilisha ofa yetu, ni siri kubwa na hatuwezi kuweka hadharani, tunasubiri jibu kutoka kwa uongozi wa Azam ili kuona tunakamilisha zoezi hilo kabla ya muda wa usajili kumalizika,” alisema Mwesigwa.

Katika kukazia hilo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na usajili wa klabu hiyo, Abdallah Bin Kleb alisema kuwa wapo katika wakati mzuri wa kumpata Ngasa.

Bin Kleb alisema kuwa kwa sasa wamefikia asilimia 85 katika majadiliano na Ngassa na kuwataka mashabiki na wanachama wa Yanga kujiandaakumpokea.

Mjumbe huyo alitoa angalizo kwa Azam FC kuwa wasilichukulie suala la usajili wa mchezaji huyo kibiashara zaidi kwani wao wanajua wazi kuwa Simba haiwezi kumsajili.

Bin Kleb alisema kama watashindwa kumsajili, basi watasubiri mwakani atakapomaliza mkataba wake na kujiunga klabu yao bila vikwazo

Post a Comment

Previous Post Next Post