SIMBA SC KUANZA KUTETEA KOMBE(LIGI KUU) SEPTEMBA 15
![]() |
Wachezaji wa Simba SC; Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu |
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, inatarajiwa kuanza Septemba 15, mwaka huu.
Kikao cha pamoja baina
ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na viongozi wa klabu za Ligi Kuu
kilichofanyika jana kimefikia uamuzi ligi hiyo ambayo kwa kawaida huanza
Septemba 1, sasa itaanza wiki ya pili ya Septemba.
Taarifa ya Ofisa Habari
wa TFF, imesema;
1. Baada ya kikao cha pamoja baina ya TFF,
Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu zote za Ligi Kuu, ilionekana kuwa kutokana
na kutokamilika kwa mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na mdhamini wa sasa,
yaani Vodacom, mwanzo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa Septemba 15, 2012. Hii
inatokana na ukweli kwamba kukamilika kwa mazungumzo baina ya pande husika,
ndio kutatoa picha halisi ya Ligi Kuu ya msimu ujao.
2. Mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na
Vodacom yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii kwa kuwa yameshafikia
hatua nzuri na hivyo mkataba unaweza kusainiwa wakati wowote baada ya
kukamilika kwa mazungumzo hayo.
3. Kukamilika kwa mazungumzo hayo ni muhimu kwa
kuwa kutasaidia Ligi Kuu kuanza bila ya matatizo yoyote kwa klabu
zinazoshiriki, TFF na Kamati ya Ligi hasa kutokana na ukweli kuwa baadhi ya
mambo yatakayokubaliwa yatalazimika kuingizwa kwenye Kanuni za Ligi; yatasaidia
upatikanaji wa fedha kwa muda muafaka; upatikanaji wa vifaa kwa muda muafaka na
masuala mengine muhimu.
4. Ratiba ya Ligi Kuu sasa inatarajiwa
kutangazwa mapema wiki ijayo pamoja na tarehe rasmi ya kuanza kwa Ligi Kuu
5. Kutokana na kusogwezwa mbele kwa tarehe ya
kuanza kwa Ligi Kuu, mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya mabingwa wa Tanzania Bara
na washindi wa pili, nao sasa utapangiwa tarehe nyingine ambayo ni wiki moja
kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu. Kwa maana hiyo mchezo huo utachezwa katika siku
itakayotangazwa baadaye.
6. Kuhusu chombo kitakachoongoza Ligi Kuu, TFF
ilitoa mapendekezo ya Kamati ya Utendaji kwa Kamati ya Ligi na baadaye kwa
viongozi wa klabu za Ligi Kuu kuhusu muundo wa chombo hicho kulingana na
mwongozo wa Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu
(FIFA) na Katiba ya TFF na suala hilo kwa sasa linajadiliwa na klabu za Ligi Kuu
kwa ajili ya hatua za mwisho
Wakati huo huo: TFF imeandaa
semina kwa ajili ya makamisaa watathmini wa marefa wa daraja la kwanza, ikiwa
ni sehemu ya maandalizi ya Ligi Kuu inayotarajia kuanza baadaye mwezi ujao.
Kwa upande wa makamisaa
na watathmini wa marefa, semina itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti
29-30 mwaka huu. Washiriki wanatakiwa kujigharamia kwa kila kitu; usafiri,
malazi na chakula wawapo kwenye semina.
Semina kwa waamuzi
itafanyika katika vituo vya Dar es Salaam na Mwanza kuanzia Agosti 31- Septemba
2 mwaka huu. Pia nao watajigharamia kwa kila tu. Waamuzi watakaoshiriki semina
hiyo ni ambao hawakushiriki ile iliyofanyika Juni mwaka huu na wale
walioshiriki lakini hawakufaulu mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness
test).
Marefa wenye beji za
Shirikisho la Kimataifa la Kimataifa (FIFA) hawashiriki kwa vile wao wamekukuwa
wakishiriki semina zao zinazoandaliwa na FIFA kila baada ya miezi mitatu.
إرسال تعليق