![]() |
| Yondan |
SIMBA SC
sasa haijitoi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, bali inatafuta njia
mbadala ya kudai haki yake ya kuporwa kwa mabavu beki wake, Kevin Yondan na wakati
huo huo kuna habari kwamba, wanachama wa Simba leo wanakwenda mahakamani
kusimamisha ligi hiyo.
Kikao cha
Kamati ya Utendaji jana, kiliamua kisiitishe Mkutano Mkuu kuwaomba wanachama
ridhaa ya kujitoa kwenye Ligi Kuu, badala yake kitafute njia nyingine ya kudai
haki.
Wakati huo
huo kuna habari kwamba wanachama watatu wa Simba leo watafungua kesi Mahakama
ya Kisutu kuomba Ligi Kuu inayoanza keshokutwa isitishwe hadi Yondan arudishwe
Simba.
Jana Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alisema kwamba Mwenyekiti
wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Wakili Alex Mgongolwa anaipotosha Ibara ya 44.3, kwa kuielezea nusu nusu
katika hukumu ya pingamizi la klabu yao dhidi ya Yanga, kuhusu mchezaji Kevin
Yondan.
Akizungumza jana, Hans Poppe ambaye ni Kapteni wa zamani wa jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), alisema kwamba Mgongolwa anapotosha na kwa ujumla Kamati yake
imekosea kumuidhinisha beki wao Yondan kuchezea Yanga, kwa kuwa klabu hiyo
haikufuata taratibu za kumsajili kulingana na maelekezo ya Ibara hiyo.
Ibara ya 44.3
kuhusu masharti maalum yanayohusu mikataba kati ya wachezaji wa kulipwa na
klabu inasema; Klabu inayotarajia kuingia
mkataba na mchezaji wa kulipwa, haina budi kuiarifu klabu yake ya sasa kwa
maandishi, kabla ya kufanya makubaliano na mchezaji huyo wa kulipwa. Mchezaji
wa kulipwa atakuwa huru tu kuingia mkataba na klabu nyingine, iwapo mkataba
wake na klabu yake ya sasa utakuwa umekwisha, au unakwisha ndani ya miezi sita,
uvunjwaji wowote wa sheria hii, utastahili vikwazo vinavyofaa.
Lakini Hans
Poppe amesema kwamba anashangaa sana kuona taarifa ya Mgongolwa inasema kwa
mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga
ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake
halali.
“Si kweli,
huyu bwana anapotosha, na mbona hakuinukuu yote Ibara hiyo katika taarifa yake?
Sasa hii ndio maana sisi tumesema, tunakutana kupanga tarehe ya Mkutano Mkuu,
kuomba Baraka za wanachama tujitoe tu kwenye ligi, kwa sababu hatutendewi haki,
haki si sahihi,”alisema Hans Poppe.
Aidha, Mwenyekiti
huyo mpya wa Friends Of Simba (F.O.S.) alisema kwamba Ibara ya 45. 6 pia
inakazia Ibara hiyo ya 44.3 na kwamba bado anashangaa kwa nini Mgongolwa,
ambaye kitaaluma ni Mwanasheria anapindisha sheria za usajili.
Ibara ya 45.
6 kuhusu Usajili na Uhamisho wa Wachezaji, inasema; Mchezaji ambaye ameingia mkataba wa zaidi ya
msimu mmoja hatoruhusiwa kujisajili na klabu nyingine, kabla ya klabu ya yake mpya kuafikiana na klabu yake ya zamani
(kanuni ya 44.3)
Mapema wiki
hii, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF pamoja na
kumuidhinisha Yondan kuchezea Yanga, iliitaka Simba kuthibitisha madai yake ya
kuingia mkataba na beki huyo na kuwasilisha upya malalamiko yake kwenye kamati
hiyo.
“Kwa mujibu
wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu
zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake halali.
Kwa vile
Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa
kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe
malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au
mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika,”alisema
Mgongolwa katika taarifa yake aliyoituma.
Mbali na
Mwenyekiti Mgongolwa, Wajumbe wengine wa Kamati hiyo waliohudhuria kikao hicho
ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo,
ambao mwishowe walipiga kura kuamua beki huyo achezee timu gani msimu ujao na
ndipo Yanga ikashinda.
Hata hivyo,
inadaiwa katika upigaji kura, tatu zilimbakisha Yondan Simba na tatu
zilimpeleka Yanga, lakini kwa kuwa Mwenyekiti ana nafasi ya kupiga kura ya
ziada, iwapo kura zimegongana- na siku hiyo Mgongolwa aliitumia kura yake
kumpeleka beki huyo Jangwani.
Katika taarifa
yake, Mgongolwa alisema kwa mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa
Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kevin Yondan,
hivyo ni mchezaji wake halali.
Alisema kwa
vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao,
imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho
iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika.
Kuhusu suala
la Mbuyu Twite, Mgongolwa alisema kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni
za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu
zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake halali.
Hata hivyo, alisema
kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na
kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku
21 iwe imelipa fedha hizo Simba.

Post a Comment