MOURINHO, REAL KUMSHITAKI BOSI WA ZAMANI WA BARCA ALIYEMWITA TAAHIRA KISA KUSHANGILIA KWA KUTELEZA KWA MAGOTI

Mourinho akishangilia kwa kuteleza kwa magoti baada ya Ronaldo kufunga goli la ushindi la Real Madrid dhidi ya Man City juzi. Real walishinda 3-2.


MADRID, Hispania
KLABU ya Real Madrid na kocha Jose Mourinho wanachukua hatua za kisheria dhidi ya mwandishi wa habari na makamu wa rais wa zamani wa Barcelona ambaye amemshambulia Mreno huyo mfululizo kwa maneno wiki hii.

Mourinho amewatumia mawakili wake dhidi ya mhariri wa michezo wa gazeti la kila siku la Marca, Roberto Palomar kufuatia habari aliyoandika iliyochapishwa katika gazeti la Jumatatu.

"Palomar ... alimtaja mteja wetu kama 'aina ya mtu ambaye atakimbia akishamgonga mtu kwa gari'," ilisema sehemu ya barua hiyo kutoka kwa mawakili wa Mourinho iliyochapishwa kwenye gazeti la leo la Marca.

"Katika macho yetu mstari huu ... haukubaliki na umetumiwa katika namna ambayo haikuwa na umuhimu wowote katika shutuma zilizotolewa."

Gazeti hilo limesema kuwa Mourinho ametaka habari hiyo ikanushwe na alipwe fidia ya euro 15,000 (Sh. milioni 30) ambazo atazitoa msaada kwa timu ya soka anayochezea mwanaye.

Katika taarifa tofauti kwenye tovuti ya klabu hiyo, Real imesema kuwa imekiagiza kitengo chao cha sheria kuchukua hatua zinazoonekana sahihi dhidi ya Alfons Godall, mkurugenzi wa Barca enzi za Joan Laporta alipokuwa rais wa klabu hiyo ya Catalunya.

Baada ya Mourinho kuteleza kwa magoti kwenye Uwanja wa Bernabeu wakati akishangilia goli la Cristiano Ronaldo katika dakika ya 90 katika ushindi wao wa 3-2 wa Ligi ya Klabu Bingwa dhidi ya Manchester City juzi Jumanne, Godall alitumia ukurasa wake wa Twitter kumshambulia Mreno huyo.

"Ni aibu taahira anashangilia goli utadhani alikuwa mchezaji," Godall aliandika.

Katika taarifa yao, mabingwa hao wa ligi walisema: "Real Madrid haitaruhusu mashambulizi ya namna hii dhidi ya wale ambao ni sehemu ya klabu klabu."

Licha ya kwamba Godall si memba wa bodi ya sasa ya Barcelona, matukio haya yatachangia uhasama baina ya miamba hao wakubwa wa Hispania  kuelekea mechi ya Real ugenini Nou Camp katika La Liga Oktoba 7.

Post a Comment

Previous Post Next Post