Jeshi la Nigeria linasema limewaua watu saba wanaoshukiwa kuwa
wafuasi wa kundi la wapiganaji wa Kiisalmu wenye msimamo mkali la Boko
Haram katika mapambano kaskazini mwa nchi hiyo.
Msemaji wa jeshi hilo amesema watu wengine zaidi
kumi na watatu wamekamatwa baada ya kushambulia kituo cha ukaguzi cha
jeshi, katika mji wa Maiduguri.
Ghasia hizo zimetokea siku moja baada ya polisi
wa Nigeria, kusema kuwa wataanza kulinda kutwa-kucha, milingoti ya simu
za mkononi kufuatia milingoti kadhaa kama hiyo kushambuliwa mwezi
uliopita, kaskazini mwa nchi.
Boko Haram ilisema ilifanya mashambulio hayo, kwa sababu milingoti hiyo inatumiwa kufuatilia mawasilino baina ya wafuasi wake.
Akitoa maelezo ya tukio hilo la Maiduguri,
Luteni Kanali Sagir Musa amesema, ''Kundi la watu wenye silaha
wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Boko Haram walishambulia kituo cha ukaguzi
cha kijeshi sehemu ambayo wanajeshi walikuwa wameweka kizuizi na kufanya
ukaguzi.
''Wanajeshi walijibu shambulio hilo kwa risasi.
Watu saba wenye silaha waliuawa katika majibizano hayo ya ufyatulianaji
risasi, na wengine kumi na watatu walikamatwa huku wengine wakikimbia.
Hakuna majeruhi waliopatikana kwa upande wa wanajeshi.''
Boko Haram wanataka kuwekwa kwa utawala wa sheria ya Kiislamu nchini Nigeria.
Kundi hilo lilianzisha kampeni ya kijeshi mwaka
2009 kupigania kuanzishwa kwa utawala wa Kiislamu, likishambulia majengo
ya serikali na makanisa na pia kuwaua wahubiri wa Kiislamu wenye
msimamo wa kati.
Nchi hiyo imegawanyika kati ya eno la kaskazini
lenye Waislamu wengi na lile la kusini linalokaliwa na Wakristo wengi na
dini nyingine.
Chanzo:-BBC Swahili

إرسال تعليق