![]() |
| Sunzu wa kwanza kushoto, katikati ni marehemu Patrick Mafisango na kulia ni Emmanuel Okwi |
SIMBA
SC jana ilifanya mazoezi yake jioni kwenye Uwanja wa Kinesi, Manzese
eneo la Urafiki, Dar es Salaam na Felix Sunzu alionyesha yeye ni mkali
katika jitihada zake za kumshawishi kocha Milovan Cirkovick ampange
kwenye mechi ya kesho, ingawa hilo linaonekana kuwa gumu.
Sunzu
alijituma sana mazoezini jana- ingawa Daniel Akuffo na Abdallah Juma
naop walifanya kazi nzuri ya kumvutia kocha Milo, ambaye kesho
anatarajiwa kuiongoza Simba SC katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu dhidi
ya JKT Ruvu.
Mazoezi
ya leo jioni ambayo yatakuwa ya mwisho kabla ya mechi ya kesho,
yanatarajiwa kuwa matamu zaidi kwa wachezaji kuonyesha uwezo wao
kumshawishi kocha awape nafasi- kumbuka kuna ushindani zaidi kwenye
nafasi ya kiungo.
Jana Milo, alikaririwa akisema kwamba anamuhitaji Sunzu, ambaye ni mchezaji ghali katika timu yake, lakini anaweza kucheza bila yeye.
Milo
alisema kwamba Sunzu hakumtumia kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara dhidi ya African Lyon kwa sababu alichelewa kurudi
Dar es Salaam kutoka kwao Zambia. “Ilikuwa kila siku anasema atakuja
kesho, kesho, haji,”alisema.
Sunzu
aliyetua Dar es Salaam siku moja kabla ya mechi na Lyon, katika kipindi
cha takriban wiki tatu hakuwa na timu, kwanza akienda kwenye msiba wa
dada yake Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na
aliporejea akaomba ruhusu ya kwenda kwao Zambia.
Alipoulizwa
kama mchezaji huyo anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko wachezaji
wote wa klabu hiyo, dola 3,500 kwa mwezi, zaidi ya Sh. Milioni 5 za
Tanzania, ni muhimu kwa sasa kwenye kikosi chake, Mserbia huyo alisema;
“Ndiyo, ni muhimu, namuhitaji, lakini naweza kucheza bila yeye,”alisema.
Inaonekana
sasa Milo anatiwa jeuri na washambuliaji wake wapya, Mghana Daniel
Akuffo, Abdallah Juma, Salim Kinje, Mrisho Ngassa na wengine ambao yupo
nao tangu msimu uliopita akina Emmanuel Okwi, pamoja na viungo wenye
uwezo wa kufunga kama Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi na wengineo.
Awali
ya hapo, Milo kwa sasa hawatumii mabeki wake wapya, Komabil Keita
kutoka Mali na Paschal Ochieng kutoka Kenya, kwa sababu anataka kwanza
waone timu hiyo inavyocheza wakiwa nje, ili wajifunze.
Profesa
huyo wa Kiserbia alisema kwamba mabeki hao wawili wa kati wanahitaji
muda kabla ya kuanza kucheza kwa mfumo wa Simba, ingawa amewasifia wote
ni wazuri.
Alisema
wakati wowote wanaweza kurudi uwanjani, iwe kwa pamoja au kupangwa na
wachezaji wengine na inawezekana hata kwenye mechi ijayo, Jumatano dhidi
ya JKT Ruvu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Aidha,
Milovan aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo wa juzi na kusema
kwamba hiyo ni zawadi kwa mashabiki wa klabu hiyo. Milo aliwapongeza
Lyon pia kwa kucheza vizuri kwenye safu ya ulinzi na kiungo kidogo na
kusema sasa anajipanga kwa ajili ya mechi ijayo ya ligi hiyo.
Lakini
Mserbia huyo hakusita kuelezea namna alivyokunwa na beki wa kati wa
Lyon, Benedictor Mwamlangala, kwa kucheza kwake vizuri kwenye mechi
hiyo.
Simba
SC Jumamosi ilianza vema kampeni za kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa mabao 3-0 African Lyon katika
mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
Milovan akiwatumia Juma Nyosso na Shomary kapombe katika beki ya kati.
Hadi
mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa
kimiani na Emanuel Okwi dakika ya 33 baada ya kuwatoka mabeki wa Lyon na
Nassor Masoud ‘Chollo’ dakika ya 36 akiunganisha krosi ya Mrisho
Ngassa.
Lyon
walikosa penalti dakika ya 35, baada ya mkwaju wa Sunday Bakari
kupanguliwa na Juma Kaseja, kufuatia Mwinyi Kazimoto kuunawa mpira
kwenye eneo la hatari.
Kipindi
cha pili, Lyon kidogo walirekebisha makosa yao, lakini bado Simba
iliendelea kutawala mchezo na dakika ya 56, Danniel Akuffo aliifungia
timu yake bao la kuhitimisha ushindi kwa mkwaju wa penalti, baada ya
Emmanuel Okwi kuangushwa kwenye eneo la hatari

إرسال تعليق