Kwa mpenzi yeyote wa Kiswahili ni sharti azingatie
stadi nne za lugha hiyo. Yaani kuzungumza, kusoma kuandika na kuelewa
lugha ya Kiswahili. Hata hivyo baadhi ya wakenya wamekuwa wakilamika
kuwa vitabu vingi vya Watanazani vimekuwa vikitahiniwa nchini Kenya
hususan katika vidato vya tatu na vinne.
Ukweli ni kuwa Watanzania wamewabwaga wakenya na
ipo mifano ya kutajika kuhusiana na hilo katika vitabu hususan vya
fasihi. Swali ni je Wakenya wamepewa fursa ya kuandika au la? Ni nani
anastahili kuwaambia waandike vitabu vya Kiswahili, na je wachapishaji
vitabu wako radhi kuzichapisha kazi za Wakenya?
Kuanzia miaka ya themanini hadi
sasa, idadi ya vitabu vya Watanzania vilivyotahiniwa katika kunga za
riwaya, tamthilia na ushairi ni kubwa kushinda vya Wakenya. Riwaya ya
Kusadikika ya Shaaban Robbert(Mtanzania) ilitahiniwa mwanzoni mwa miaka
ya tisini hadi mwaka 1994. Wakati huo hadi mwaka 1997 tamthilia ya
Mashetani ya Ebarahim N. Hussein(Mtanzania) ilitahiniwa. Mwaka wa 1994
hadi mwaka 1998 riwaya ya Kisima cha Giningi ya Mohamed Said
Abdullah(Mtanzania) ilitahiniwa. Katika miaka hiyo kuanzia mwaka 1998
tamthilia ya Amezidi ya Said Ahmed Mohamed (Mpemba) ikaanza kutahiniwa
kuchukua mahali ya tamthilia ya Buriani ya A. S Yahya na David
Mulwa(Wakenya). Wakati huo Mkenya Khaemba Ongeti alijipenyeza na
tamthilia yake ya Visiki.
Hayakuishia hapo, baada ya tamthilia za Visiki
na Amezidi kuondolewa katika ratiba ya shule za upili nchii Kenya
ikaingia riwaya nyigine ya Mohamed Said Ahmed (Mpemba) ya Kitumbua
kimeingia mchanga. Na hiyo ilipoondoka ikaja riwaya ya Utengano ambayo
inatahiniwa hadi sasa.
Ukweli unaojitokeza hapa ni kuwa taasisi ya
elimu nchini haiviteui vitabu hivyo kwa sababu ni vya Watanzania. Ni
kutokana namna vilivyosukwa kimaudhui na kifani. Isitoshe waandishi wa
vitabu hivyo wameandika wameandika vitabu vingi tu. Kwa mfano Said Ahmed
Mohemed ameandika zaidi ya vitabu 40 vya Kiswahili. Mohamed Said
Abdullah ameandika vitabu vingi tu kama vile Kisima cha Giningi, Duniani
kuna watu, Mizimu ya watu wa kale na Kadhalika.
Hata hivyo ni vyema kutambua kuwa baadhi ya
Wakenya wamejitokeza na kuandika kazi nzuri za fasihi ya Kiswahili kama
vile Siku Njema ya Ken Walibora, Mstahiki Meya ya Timothy Arege na Kifo
Kisimani ya Kithaka Wamberia. Kwa ufupi wapenzi wa Kiswahili katika
kanda ya Afrika Mashariki wakijumuisha mataifa ya Rwanda, Sudan Kusini,
Sudan, Somalia na Uganda waandike vitabu zaidi vya Kiswahili. Twasubiri
siku watanzania watavitahini vitabu vya Kiswahili vya wakenya, Vivyo
hivyo si dhambi kitabu cha Kiswahili kilichoandikwa na Mrundi ama
Mnyarwanda kikitahiniwa Uganda na vinginevyo. Ni maoni tu!
Chanzo:- http://www.bbc.co.uk
إرسال تعليق