Jakob Michelsen |
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface
Wambura amesema leo kwamba, Serengeti Boys ambayo iko chini ya
Kocha Mdenmark, Jakob Michelsen itacheza mechi hiyo ya raundi ya tatu na
mshindi kati ya Congo Brazzaville na Zimbabwe ambapo tayari Congo Brazzaville
imefanikiwa kupata ushindi wa ugenini wa mabao 2-1. Mechi ya marudiano
itachezwa jijini Brazzaville kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu.
Katika mechi hiyo ya raundi ya tatu, Serengeti Boys itaanzia
nyumbani katika mchezo utakaofanyika Novemba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa
Taifa, wakati mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye.
Wambura amesema TFF ipo katika mikakati ya kuhakikisha
Serengeti Boys inapata mechi mbili za kirafiki za kimataifa kabla ya kumvaa
mshindi kati ya Congo Brazzaville na Zimbabwe. Fainali za Afrika kwa vijana
wenye umri chini ya miaka 17 zitafanyika Machi mwakani nchini Morocco.
Tanzania imefuzu bila jasho hadi kufika hatua hiyo, baada ya
wapinzani wake wa awali, Kenya na Misri kujitoa katika Raundi ya Kwanza na ya Pili.
Kama Tanzania itafuzu kushiriki Fainali hizo za mwakani,
itapoza machungu ya mwaka 2005 walipofuzu kucheza Fainali za Vijana wa umri huo
kwa kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe, lakini baadaye kwa sababu ya ‘kufoji’
umri wa Nurdin Bakari, ikaondolewa mashindanoni.
Zaidi ya Fainali za Mataifa ya Afrika 1980 na CHAN 2009,
katika soka ya wanaume, Tanzania haijashiriki fainali nyingine zozote za Afrika
tangu iingie kwenye soka ya kimataifa.
إرسال تعليق