Ukweli ni kwamba kuna viongozi wa juu kwenye serikali ya Zanzibar ambao
kwa kushirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania wanahusika
moja kwa mja kwenye machafuko ya Zanzibar kuanzia yale ya kwenye
uchaguzi mdogo wa Bububu hadi haya sasa.
Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba ajenda ya Wazanzibari kudai mamlaka
kamili kupitia mchakato wa Katiba Mpya inashindwa kwa kuiua kabisa
serikali ya Umoja wa Kitaifa na Maridhiano.
Makubaliano ya pamoja kati ya Dodoma, kundi la vibaraka wao kwenye GNU
na CCM Zanzibar na Idara ya Usalama wa Taifa, ni kwamba Maridhiano
yaliyozaa GNU ndio adui nambari moja wa mfumo wa Muungano uliopo. Sasa
ili kuulinda mfumo huu wa Muungano, ni lazima kumuangamiza adui huyo. Na
ndicho kinachofanyika sasa.
Tukio la kutekwa kwa Ustaadh Farid lilikuwa la kweli na lilikuwa ni
sehemu ya programu hiyo kubwa ambayo inagharimu mamilioni ya fedha za
walipa kodi wa Tanzania nzima na si wa Zanzibar peke yake. Kiasi cha
mwezi mzima kabla ya Ustaadh Farid kutekwa, kijana mmoja wa Idara ya
Usalama wa Taifa anayefanya kazi Zanzibar, alijenga mahusiano makubwa na
viongozi wa juu wa Uamsho, hasa Sheikh Farid.
Kijana huyu, ambaye hakujificha kwamba ni mtu wa Usalama wa Taifa,
alijitokeza kama sehemu ya kundi la watu waliomo kwenye taasisi za dola
na ambao wanaunga mkono Ajenda ya Zanzibar. Kwa maslahi ya ajenda hiyo,
na kwa maslahi ya Zanzibar, bahati mbaya viongozi wa Uamsho
walimuamini.
Ni yeye ndiye aliyekuwa mtu wa mwanzo kabisa kumpigia simu Sheikh
Msellem saa 2:00 usiku wa siku ya kutekwa kwa Imamu Farid, kumjuulisha
kwamba Usalama wa Taifa wamemkamata Sheikh Farid.
Ndani ya siku tatu za suintofahamu hiyo, ni yeye aliyekuwa
akiwashinikiza viongozi wa Uamsho na vijana kwamba ni lazima shinikizo
kubwa lifanyike kama kweli wanataka kiongozi wao aachiwe akiwa salama.
Kwa hakika, siku ya pili yake aliwasiliana na kukutana na Sheikh
Msellem, na kumuambia kwamba alikuwa tayari kumpeleka aliko Sheikh
Farid. Baada ya kuingia kwenye gari, hakumpeleka kwa Sheikh Farid, bali
alimwambia kwamba wazungumze naye kwa simu kwanza, akiwa tayari
ameshaipiga simu hiyo, kwa alivyosema.
Kwenye simu, ni kweli Sheikh Msellem alisikia sauti ya Sheikh Farid
ikimuambia kwamba ametekwa na wanamtesa, na kwamba kama hawakujikaza
basi wanaweza hata kumuua. Alipotaka kuuliza mengi zaidi, Sheikh Msellem
hakuweza maana ile simu ilikatwa.
Kumbe kilichokuwa kimefanyika, ni kuwa Sheikh Msellem alisikilizishwa
sauti ya kurikodi ya Sheikh Farid na hakuwa anazungumza naye moja kwa
moja. Ilikuwa ni baadaye sana, viongozi wa Uamsho walipokuja kung’amua
hayo.
Ndani ya kipindi hicho cha kupotea kwa Ustaadh Farid, viongozi wa
serikali ya Zanzibar wanaohusika na programu yao, waliyatoa makundi ya
vijana wao kuchoma maskani za Kisonge, kuharibu mali, kuiba, kupiga,
kujeruhi, na hata kuua.
Katika purukushani hizo, vijana hao walikuwa wakipigana na kuumizana
wenyewe kwa wenyewe. Miongoni mwao ni askari aliyepigwa risasi na kuuawa
na wenzake, lakini huyo hatajwi kabisa na vyombo vya habari, badala
yake anatajwa askari aliyeuawa Bububu kwa kukatwa mapanga, na ambaye
huenda kabisa asiwe na uhusiano na matukio haya.
Miongoni mwa vijana walioumizwa wako waliojeruhiwa vibaya na ambao hadi
sasa wamelazwa kwenye hospitali ya jeshi ya Bububu, lakini taarifa zao
zimewekwa siri sana. Kilichotokea, ikiwa ni sehemu ya programu hiyo
kubwa, ni kwa Idara ya Habari Maelezo ya SMZ kutoa agizo kwa vyombo
vyote vya ndani vya habari kutokutangaza kabisa matukio ya sasa, tangu
kukamatwa kwa Sheikh Farid.
Kwa hakika, hata katika kamatakamata ya polisi, nao pia wamewakamata
vijana kadhaa wa makundi hayo lakini huwa wanawaachia kwa amri ya
Kamishna Mussa Ali Mussa, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Zanzibar, ambaye ni
sehemu ya programu hiyo ya kuivunja GNU.
Sheikh Farid aliachiliwa baada ya uingiliaji kati viongozi wawili wa juu
GNU, kwa kuanzia na Makamo wa Kwanza wa Rais Seif Sharif ambaye baada
ya kufahamishwa undani wa mkasa mzima alimwendea Rais Ali Shein, na
kumuambia maneno yafuatayo: “Mhe. Rais ninasikitika sana kwamba sisi
wenyewe ndio tunaohusika na haya yanayotokezea hivi sasa. Watu wetu
wanajua wapi alipo Sheikh Farid. Wanafanya hivi kukuharibia wewe
uonekane kwamba huna uwezo wa kuongoza na kwamba unaiwachia nchi iingie
kwenye machafuko. Lakini zaidi wanafanya hivi ili kuivunja GNU, maana
watatufanya sisi tujihisi kwamba ni sehemu ya uozo huo nasi
hatutakubali. Sasa waambie watu wako ambao wako chini ya ofisi yako
(akamtaja kwa jina yule kijana wa Idara ya Usalama wa Taifa) wakuoneshe
walipomueka Farid.” Usiku wake, saa 2:00 Sheikh Farid akaachiliwa.
Lakini hadi kuachiliwa kwa Sheikh Farid, tayari sehemu ya lengo moja
kwenye mkakati wao ilishafanikiwa: nayo ni kutengeneza mazingira ya fujo
na kuhalalisha matumizi ya nguvu, ghasia na uvunjwaji wa haki za
binaadamu kama yanayoendelea sasa.
Pia kwa sababu ya kuficha uovu na asili ya mkasa mzima, wamemkamata
Sheikh Farid na viongozi wa Uamsho ambao wanaujua ukweli wote wa mkasa
huu, na sasa wamewaweka ndani na kuwafungulia mashitaka kadhaa, ili
wasiwe nje wakaweza kuueleza umma kile hasa kilichotokea.
Kwa upande mwengine, wanavilisha vyombo vya habari vya Tanzania Bara na
vile vya Zanzibar vinavyopinga Maridhiano na Umoja wa Kitaifa, taarifa
za uongo kuhusu viongozi hao wa Uamsho na wafuasi wao. Picha inayojengwa
ni kwamba Uamsho ni magaidi na hivyo wapate kuhalalisha kuongeza
wanajeshi na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola dhidi ya raia wanaodai
mfumo wa Muungano wa Mkataba.
Hivi sasa operesheni ya kijeshi imeimarishwa kisiwani Unguja, hasa
kwenye mkoa wa Mjini Magharibi, ambako Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba
Mpya inakuja hivi karibuni. Wananchi wanatishwa na wanatiwa hofu na
mazingira yanajengwa ya kuzuia maoni ya wananchi hao mbele ya Tume,
maana hadi sasa wengi waliokwishatoa maoni yao, wameshasema wazi
wanataka mabadiliko ya msingi kwenye Muungano.
Matokeo wanayoyatarajia ni aidha kwa wananchi wanaopigwa na makundi
waliyoyatayarisha na vikosi vya SMZ kujibu mapigo na hivyo kuiingiza
nchi moja kwa moja kwenye fujo za kudumu, au kwa wajumbe wa CUF kwenye
GNU kuja juu na kujitoa kwa kupinga dhuluma hii. Lolote kati ya mawili
hayo, mwisho wake ni kuyavunja maridhiano na umoja wa kitaifa na hivyo
kuiua na kuizika kabisa Ajenda ya Zanzibar.
Kwa upande wa wananchi, programu hiyo inalenga kuwavunja moyo wao kwa
serikali ya GNU, hasa kwa wafuasi wa CUF mbele ya Makamo wa Kwanza Seif
Sharif, ambaye wanajengewa picha ya kwamba amewasaliti na haguswi na
mateso wanayoyapata.
Mwenyewe Maalim Seif analijua na analifuatilia kwa karibu kila
linalotokea na anamshauri Rais Shein kama ulivyo wajibu wake kama makamo
wa kwanza wa Rais. Amechukua na anaendelea kuchukua kila jitihada za
kumsaidia Rais Shein na kuilinda GNU isianguke, maana ikianguka ndio
hatima ya Zanzibar imekwenda pamoja nayo.
Katika ghasia zinazoendelea sasa kwenye jimbo la Bububu, amemfahamisha
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayehusika na vikosi vya SMZ, Dkt.
Mwinyihaji Makame, na amemueleza wazi kwamba kinachofanyika ni uvunjaji
wa haki za binaadamu, mateso na udhalilishaji, ambao mwisho wake ni kwa
wananchi kuamua kujilinda na machafuko yakisambaa, hakuna hata mmoja
atakayenusurika, si Dkt. Mwinyihaji wala si yeye Maalim Seif.
Laiti Rais Ali Mohammed Shein ana dhamira, nia na uwezo wa kuinusuru
ndiye mwenye nafasi ya juu kufanya hivyo. Wapinzani wa Maridhiano na
Umoja wa Kitaifa walikuwapo pia wakati wa muasisi wake, Rais Amani
Karume, lakini alikuwa na uthubutu wa kuwadhibiti.
Rais Shein kwa upande ake anaonekana kuelemewa vibaya na kundi la
wapinzani wa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa waliomo kwenye serikali
yake, chama chake na vyombo vyake vya usalama. Kundi hilo ambalo
linatumikia ajenda ya Tanganyika dhidi ya Zanzibar, kama ilivyoonekana
wazi, liko tayari hata kukanyaga maiti za Wazanzibari alimradi tu
lifikie kwenye lengo lake.
Kwa hivyo, inabakia kuwa juu ya Wazanzibari ambao sasa wanateseka chini
ya mikono ya kundi hilo aidha kulipa nafasi ya kumaliza kazi liliyoianza
ya kuisimamisha ajenda ya Tanganyika, au kuyapa nafasi Maridhiano na
Umoja wa Kitaifa nayo kumaliza kazi yaliyoianza ya Ajenda ya Zanzibar.
Zanzibar imeanza tena kuzama. Inahitaji kuokolewa hivi sasa.
Chanzo. mzalendo.net

إرسال تعليق