Kocha wa Thierry alivyouawa kikatili

Kocha Michael Jones
NEW YORK, MAREKANI
JUMAPILI iliyopita, aliyekuwa nyota wa Arsenal, Thierry Henry alijaa huzuni kwa sababu mdau wa soka katika klabu yake Michael Jones alifariki dunia.

Kifo humpata kila binadamu tena wakati wowote lakini kuna aina ya vifo ambavyo huhuzunisha zaidi. Ndiyo maana Henry ilikuwa na huzuni baada ya Jones kufa kikatili.

Henry na Jones walifahamiana tangu England na walijikuta wakiitumikia klabu moja ya New York Red Bull, mmoja akiwa mchezaji na mwingine akiwa kocha wa vijana.

Wawili hao walikuwa wakikutana mara kadhaa wakati walipokuwa wakifanya matamasha ya vijana au wakati Henry alipotakiwa kujumuika na vijana kwa ajili ya kuwapa hamasa ya kuendelea na soka. Mara kadhaa Henry alikuwa akifika katika viwanja vya watoto na kupiga nao picha au kuwakumbusha baadhi ya sheria za soka.

Lakini, Jones hayupo tena aliuawa kikatili, Jumapili iliyopita.
Michael Jones mzaliwa wa Liverpool, England aliuawa kwa kuchomwa kisu mara kadhaa kwenye kifua na shingo yake ikakatwa na mtu asiyejulikana Jumapili iliyopita majira ya saa 10:30 alfajiri huko New York, Marekani.

Majirani wa Jones wamesema kuwa awali kocha huyo alionekana akizungumza na mtu mmoja kwa hasira na baadaye waliondoka pamoja. Lakini baadaye wakapata taarifa kwamba Jones ameuawa kikatili. Muuaji alimchoma kisu kifuani na kisha kumchinja, kama hiyo haitoshi alimkata masikio. Baada ya hapo akamtupa pembeni mwa barabara.

Polisi waliitwa na walimpeleka hospitalini ambapo daktari alithibitisha kifo chake. Majirani wamewaambia polisi kwamba mtu aliyekuwa akizozana na Jones kabla ya kifo chake, alikuwa mrefu na alikuwa na nywele nyingi nyeusi.

Kifo cha Jones si tu kwamba kimesikitisha Henry bali pia uongozi mzima wa klabu kwa kuwa kocha huyo alikuwa na mipango mizuri ya kuhakikisha anakuza soka la vijana.

"Alikuwa kocha mzuri ambaye alipenda soka na alikuwa na marafiki wengi," ilisema taarifa kutoka Red Bull.

"Taarifa hizo ni mbaya kwa jumuiya ya Red Bull. Tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunawasidia polisi kufanya uchunguzi wa kina na kumbaini muuaji."

Kituo cha televisheni cha WABC kimetoa taarifa kwamba polisi wanadhani mauaji hayo ni ya kulipa kisasi na wala muuaji hakuwa na nia ya kuiba. Polisi wametoa maelezo hayo ya awali kwa sababu mhusika alikutwa na simu yake na pochi ndogo ya kuhifadhia fedha.

Post a Comment

أحدث أقدم