Kamanda Barlow
Mwanza
Siku moja baada ya Jeshi la Polisi kutoa taarifa
ya awali ya uchunguzi wa mauaji ya kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kwa
ajili ya kutekeleza mauaji hayo imenaswa.
Kamanda Barlow aliuawa usiku wa manane alipokuwa
akitoka kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake. Alifikwa na mauti hayo
baada ya kupigwa risasi akimsindikiza Mwalimu Doroth Moses.
Habari zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya
makachero jijini Mwanza zinaeleza kuwa, ukweli wa mauaji hayo umebainika
na kwamba watuhumiwa waliokamatwa wanahusika moja kwa moja na mpango
kamili wa mauaji hayo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, inadaiwa kuwa Kamanda
aliuawa baada ya mmoja wa wahalifu aliyekuwa akikabiliwa na kesi nzito
(jina tunalihifadhi) kutoa kiasi cha fedha kupitia kwa mtu wake wa
karibu ili kutekeleza mpango wa mauaji ya kulipiza kisasi.
Kupatikana kwa wauaji hao, kumetokana na simu ya Mwalimu Dorothy Moses kupitia ujumbe wa simu aliokuwa akiwasiliana na wahusika.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Lilian Matola alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alisema
taarifa siyo za kweli na kusisitiza kwamba taarifa aliyoitoa DCI Robert
Manumba ndiyo sahihi.
"Haya mambo yanatoka wapi, kwanza siyo kweli hata kidogo, hawa
ni watu walikuwa kwenye safari zao za uhalifu ndipo wakakutana na
Kamanda Barlow," alisema.
Habari hizo zinaeleza kuwa, kubainika kwa mpango
huo ni baada ya kunasa ujumbe mfupi wa maandishi uliokuwa ukionyesha
matukio yote tangu walipokuwa hotelini na kwamba wakati wote wauaji
walikuwa wakipewa taarifa za kila nyendo za Kamanda Barlow.
Ujumbe mmojawapo ulionaswa katika moja ya simu unasema, “Nipo kijiweni kwangu…. nitawajulisha zaidi”.
Alisema kutokana na kubainika kwa ujumbe huo wa
maandishi wa simu, jeshi hilo limelazimika kufuatilia matukio kadhaa
yaliyomo katika historia ya mtuhumiwa.
Kuhusu kauli ya Manumba alisema kuwa, kama DCI
Manumba alitoa taarifa yake kwa lengo la kiintelejensia kwa ajili ya
kusaidia upelelezi anakubaliana na hilo.”
“Unajua kuna mbinu nyingi za upelelezi,
inawezekana wameeleza hayo ili kuwazubaisha watuhumiwa kisha uchunguzi
wa kina ukaendelea, hapo ni sawa, lakini kama ndiyo mwelekeo wa
uchunguzi wao, basi wanapaswa kujua kuwa wameacha vitu vingi sana vya
msingi,” alieleza askari mwingine.
DCI Manumba katika taarifa yake, alisema kwamba
Jeshi la Polisi limewatia mbaroni watu watano jijini Dar es Salaam
wakiwa na bunduki aina ya shortgun inayodaiwa kutumika katika mauaji
hayo. Hata hivyo walishindwa kubainisha sababu za mauaji hayo licha ya
kueleza kuwa watuhumiwa waliokamatwa walikiri kuhusika.
Alisema, mbali na kuwakamata watuhumiwa hao watano
na kukiri pamoja na kuonyesha bunduki aina ya shortgun waliyotumia kwa
mauaji, watuhumiwa wengine wawili bado wanasakwa pamoja na redio ya
mawimbi ya kamanda huyo ambayo iliibiwa eneo la tukio yalikotokea mauaji
Akielezea chanzo cha mauaji hayo kutobainika, Inspekta Generali
wa Polisi, IGP, Said Mwema alisema jeshi lake pamoja na kuwakamata watu
watano jijini Dar es Salaam wanaosadikiwa kuwa majambazi, bado
wanafanya uchuguzi wa chanzo cha mauaji hayo ili kujua kama majambazi
hao walikutana na kamanda kwa bahati mbaya katika kazi zao au la.
Chanzo: Mwananchi
إرسال تعليق