
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, John Samwel Malecela
akimtunuku Shahada ya Uongozi wa Biashara, Mke wa Waziri Mkuu, Mama
Tunu Pinda katika Mahafali ya Chuo Kikuu Huria yaliyofanyika kwenye
viwanja vya Chuo hicho Kibaha Oktoba 27, 2012.Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu
----
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amewataka Watanzania wahakikishe kuwa wao wenyewe na watoto wao
wanatumia fursa ya kudahiliwa kwenye Chuo Kikuu Huria badala ya
kuendelea kusubiri mabweni yajengwe kwenye Vyuo Vikuu.
“Kama tutasubiri mashirika na
taasisi za dini au watu binafsi wajenge vyuo vikuu vya mabweni, ni
dhahiri wanafunzi wengi wasio na uwezo wa kulipia ada katika vyuo hivyo
watasubiri kwa muda mrefu ili wadahiliwe au wakose kabisa nafasi kwenye
Vyuo Vikuu,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
jana jioni (Jumamosi, Oktoba 27, 2012) wakati akiwahutubia washiriki wa
mahafali ya 20 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yaliyofanyika
kwenye viwanja vya chuo hicho eneo la Bungo, wilayani Kibaha, Pwani.
Alisema kuwepo kwa Chuo Kikuu
Huria kumetoa fursa ya kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vikuu
kwa kiwango kikubwa kwa vile kinaweza kuchukua wanafunzi wengi kwa
wakati mmoja.
“Napenda kuwasihi wananchi
kujiunga na chuo hiki kutokana na ubora wa elimu inayotolewa pamoja na
uhakika wa kuendelea na shughuli za kazi, ajira binafsi na kumwezesha
mtu kukaa pamoja na familia,” alisema.
Waziri Mkuu aliahidi kufuatilia
ombi la ujenzi wa barabara ya lami iendayo kwenye chuo hicho ambayo
haizidi kilometa nne ili ikamilike mapema. Pia alimtaka Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ashirikiane na Wakala wa
Majengo (TBA) kuharakisha upatikanaji haraka wa majengo mikoani kwa
taratibu zinazokubalika ili yasaidie kutatua tatizo la vituo vya
kufundishia wataalamu mikoani.
Jumla ya wahitimu 2,787
walitunukiwa vyeti, stashahada, shahada za kwanza, na stashahada za juu
katika fani za Sayansi ya Jamii, Ualimu, Elimu Maalum, Biashara na
Fedha, Sayansi, Sheria, Uhasibu, Uchumi, Mazingira, Utalii, Masoko,
Kiswahili, Utawala, Uandishi wa Habari na Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano.
Miongoni mwa viongozi
waliohitimu jana ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda aliyehitimu
Shahada ya Uongozi wa Biashara na Biashara ya Kimataifa (BBA –
International Business). Wengine ni wakuu wa mikoa ya Shinyanga na
Simiyu, Bw. Ali Nassoro Rufunga na Bw. Pascal Mabiti wakiwemo pia Mkuu
wa Wilaya ya Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla na Mbunge wa
Tandahimba, Bw. Juma Njwayo.
Akihojiwa na waandishi wa habari
mara baada ya kupatiwa shahada yake, Mama Tunu Pinda alisema anawasihi
wanawake wote wajiendeleze bila kujali wako kwenye nafasi ipi kwani
elimu haina mwisho. “Umuhimu wa elimu hauangalii kama wewe ni mke wa
kiongozi au la, elimu inawahusu watu wote!,” alisema.
Alisema mahafali hayo yamempa
hamasa ya kusoma tena zaidi na zaidi kwani ameona wahitimu wengine
wakipata shahada za juu zaidi. “Nimeona wenzagu wakipokea Ph.D zao
nikasema mimi nina Bachelor tu, hapana. Lazima niende mbele zaidi,”
alisema bila kufafanua kuwa atasomea fani gani.
Mapema, Mwenyekiti wa Baraza la
Chuo hicho, Prof. Samwel Wangwe alisema Chuo hicho tayari kinashirikiana
na vyuo vingine vya elimu ya juu vya umma hapa nchini kama SUA, MUHAS,
DIT na CBE ili kuongeza udahili wa wanafunzi vyuoni.
Alisema chuo hicho kina mpango
wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kwa kuchapisha vitabu vya
kujisomea kwenye CD na DVD ili kupunguza gharama za uchapishaji wa
vitabu.
Aliziomba wizara zenye majengo
yasiyotumika huko mikoani ziyatoe kwa chuo hicho ili yafanyiwe ukarabati
na yaweze kutumika kutoa elimu kwa wataalam wengi zaidi nchini.
Alitumia fursa hiyo kuiomba
Wizara ya Ujenzi waiingize barabara iendayo stesheni ya Soga kupitia
chuoni hapo katika mpango wake wa muda mfupi ili iwekewe lami na hivyo
kurahisisha mawasiliano kwa wakazi wa eneo hilo.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho,
Prof. Tolly Mbwete alisema Chuo hicho kina eneo la ekari 105 na kwamba
kinatarajia kuanza ujenzi wa majengo mawili kwa ajili ya madarasa na
ofisi za chuo ambao utagharimu sh. bilioni 15/-.
Kuhusu changamoto zinazokikabili
Chuo hicho, Prof. Mbwete alisema wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa
rasilmali fedha, uhaba wa mabweni na uhaba wa wanataaluma. Aliomba
wapatiwe fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu yake. Aliomba kuwe na
ushirikiano wa karibu zaidi na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma ili wapatiwe fedha za malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wa
chuo hicho.
إرسال تعليق