Askari wa kutuliza ghasia (FFU), wakiwa katika doria aneo la darajani
Zanzibar jana ili kukabiliana na wafuasi wa Sheikh Farid Hadi Ahmed,
wanayedai kutekwa na watu wasiojulikana katikati ya wiki hii, vyombo
vya dola vimekanusha kuhusika na kutekwa kwa kiongozi huyo
Askari wa kutuliza ghasia (FFU),wakiwa wamemtia nguvuni, mmoja wa watu,
wakati wa vurugu baina ya kundi la uamsho la Zanzibar na polisi eneo la
Darajani Unguja jana, wakidai kuachiwa kwa kiongozi wao sheikh Farid
Hadi Ahmed, nayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana. vyombo vya dola
vimekanusha kuhusika na kutekwa kwa kiongozi huyo
Na Salma Said
VURUGU zimeendelea
Zanzibar huku mtu mmoja akiuawa baada ya kupigwa risasi ya moto na
askari wa Kikosi cha Valantia (KVZ) usiku wa kuamikia jana. Habari
za kuaminika zinasema mtu huyo, Salum Hassan Muhoja mwenye umri wa
miaka 30 mkazi wa Regeza Mwendo nje kidogo ya mji wa Zanzibar alipigwa
risasi karibu na Amaan mjini hapa.
Inaaminika kuwa mtu huyo alipigwa risasi wakati akipita karibu na baa na nyumba yakulala wageni Mbawala Amaan ambayo ilivunjwa katika ghasia hizo. Kijana huyo alitarajiwakuzikwa jana jioni kijijini kwao Mwera Regeza Mwendo wilaya ya Magharibi Unguja.
Wakati kukiwa na habari
hizo za mauaji vijana kadhaa wenye umri wa kati ya miaka 14 na 18
waliingia barabarani eneo la Darajani na kupambana na askari ambao
walikuwa wametanda wakilinda doria.Vijana
hao huku wakiimba “tunamtaka amiri wetu , tunamtaka amiri wetu,
tunamtaka amiri wertu” walitawanywa na askari hao huku wakirusha mawe
kwa askari hao.
Hali hiyo iliwafanya
polisi kupiga ovyo mabomu ya machozi katika mitaa ya Zanzibar huku
wakifyatua risasi za moto na kuufanya mji kuhanikiza kwa vishindo vya
mabomu na risasi na kuzifunga barabara kadhaa.
Baada ya sala ya Ijumaa
katika misikiti mbalimbali hali ilonekana kuwa tulivu mjini hapa huku
askari wakiwa wamejaa mitaani wakiwa kwenye magari na wengine wakitembea
kwa mgguu wakiwa wameshikilia bunduki.
Katika baadhi ya misikiti
wakati wa sala ya Ijumaa ilisomwa dua marufu ya Kunuti ikiwa ni sehemu
ya kuiombea amani nchi kutokana na vurugu hizo.
Hali ilianza kuchafuka saa
8 mchana wakati kikundi cha vijana kilichokuwa kimejikusanya eneo la
Uwanja wa Malindi kuingia barabarani huku wakipiga kelele za kumtaka
amiri wao, Farid Hadi Ahmed ambaye alitoweka tangu Jumanne iliyopita.
“Kupotea” kwa sheikh huyo
ndiko kulikozua ghasia mjini hapa tangu Jumatano na kufanya mji
usikalike huku biashara zote zikiwa zimefungwa na askari mmoja kuchinjwa
Jumatano usiku.Wafuasi wa Sheikh huyo wanaamini kwamba kiongozi wao amekamatwa na serikali kwa hiyo wanashinikiza ili aachiwe huru. Barabara
za mjini hapa zimejaa takakataka za kila aina kuanzia vifusi, mawe
makubwa, matairi yaliyochomwa moto, matofali na vifuu vya madafu na
kuharibu miundombinu kadhaa zikiwemo kukata waya.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi,
Said Juma Hamis alisema kuwa hana taarifa za kuuawa kijana huyo zaidi ya
zile za kuuawa kwa skari wao Bububu.Alisema kwamba jeshi lake litafuatilia kwa karibu juu ya tukio hilo ili kujua ukweli wake,
Kamanda
Hamis alisema kuwa hadi jana jumla ya watuhumiwa waliokamatwa kutokana
na vurugu hizo ni 39 huku wanane walifikishwa mahakamani jana na wengine
wanaendelea kuhojiwa na Polisi. Kaimu
Kamanda huyo pia alisema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi
zake za kumtafuta kiongozi huyo wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu,
Sheikh Farid ambae anadaiwa kutekwa.
Alisema
kuwa katika kufanikisha juhudi hizo jana kulifanyika kikao cha
wapelelezi kilichoongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi
Zanzibar, ACP Yussuf Ilembo kujadili namna gani wanaweza kumpata au
kujua yupo wapi Sheikh huyo.
Vipindi vya Uamsho vyapigwa marufuku
Katika
hatua nyingine Tume ya Utangazaji ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imepiga marufuku vipindi vyote kwenye redio na televisheni vya kikundi
cha dini cha Uamsho.
Barua
iliyotumwa jana kwa Wakurugenzi wa vituo vya redio na televisheni vya
hapa ilisema kwamba hatua hiyo imetokana na ghasiza zinazoendelea nchini
ambazo inasadikiwa kuwa zinachochewa na kikundi hicho.
Barua
hiyo iliyosainiwa na Mtumwa B Mzee kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume
ya Utangazaji ilisema kwamba itawachukulia hatua wale wote watakaokaidi
agizo hilo.
Waandishi wako katika hatari
Waandishi
wa habari waliopo mjini Zanzibar wanaofuatilia ghasia zinazoendelea
hapa wamekuwa kwenye hatari kwa kutishiwa maisha yao na vijana
wanaofanya vurugu. Makundi
yanayofanya vurugu yako ya aina tatu Ubaya ubaya, Kimya kimya na Mbwa
mwitu hufanya vurugu na kupora watu mali zao wakiwemo kwenye vyombo vya
usafiri na kuvamia mabaa.
Waandishi
hao wakiwemo wa kimataifa walivamiwa na kundi la vijana na kuwekwa
chini ya ulinzi eneo la Mbuyuni na kutaka kunyang'anywa vifaa vyao vya
kazi lakini waliokolewa na walinzi waliokuwa jirani.
Waandishi
walivamiwa katika eneo la Mbuyuni baada ya kumaliza kusali sala ya
Ijumaa ambapo waandishi hao walitakiwa kuondoka na kutishiwa maisha yao
kwa kupigwa ambapo baadhi yao walisukumwa na kupigwa.
“Mimi
nimeshachoka kupigwa na hawa watu lakini niliyempiga ninamjua na kwa
kweli kwa sasa hatukubali tena” alisema Munir zakaria mwandishi wa
Channel Ten.
Vipeperushi vyasambazwa Zanzibar, vya watia khofu wakristo
Vipeperushi
vinavyotishia uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar
vimepeperushwa mjini hapa kufuatia ghasia zinazoendelea kwa siku ya tatu
mfululizo.
Kipeperushi
kimojawapo kinasema: “CCM kosa letu kuwatia mbwa msikitini. Sasa
tunasema kuwa basi tena litakalokuwa na liwe kwa sisi CCM basi tena
umoja na CUF.
Nyie
CUF/Muamsho Abubakari Khamis Bakar (Waziri wa Katiba), Mussa (Kamishna
wa Polisi) na Azizi (Kamanda wa Polisi Mkoa) mmeshazoea fujo na sisi
sera yetu CCM sera yetu amani sasa mujiuzulu mumpishe Rais afanye kazi
zake, Tumechoka na nyinyi juu ya mauaji ya askari wetu. Ondokeni murudi
kwenu.
Wewe
Abubakar hukuanza leo na jana ufisadi kazi ya ufisadi umeizoweya hadi
ulifungwa jela na mafisadi wenzako, mwishowe huku SMZ kumekuokoa.”
Wakati
huo huo kuna waraka umesambazwa ambao umewatisha khofu waumini wa dini
ya kikristo nchini ukisema wote watakatwa vichwa waraka huo ambao
unasemekana umetolewa na watu wenye kujiita jumuiya ya Uamsho umeandikwa
na kusambazwa katika maeneo mbali mbali huku wenyewe wakristo
wakipelekewa maofisini kwao.
Akizungumza
na masikitiko Askofu wa Kanisa la Anglikan Mkunazini Emmanuel Masoud
amesema ni wakara ambao umewastusha wakristo kutokana na maneno mazito
yalioandikwa humo ambapo ndani ya wakara huo.
“Maneno
yaliandikwa humu yametushitua sana wiwi waumini wa dini ya kikristo
hapa Zanzibar kwa kwa kweli sio jambo la kupuuzia ikiwa wanasema
watatukata vichwa ni jambo la hatari kabisa” alisema Masoud.
Wakizungumzia
ukweli juu ya suala hilo Sheikh Azzan amesema jumuiya yake haihusiki na
waraka wa aina hiyo na wao kama waislamu hawana sababu ya kuwatisha
watu kwa kuwa wanaamini uislamu sio dini ya kuwabagua watu wala
kuwatisha watu.
Azzan
alisema wapo baadhi ya watu ambao wanatumia propaganda mbaya za kutaka
kuwagawa wazanzibar katika kipindi hiki na ndio wanatumia kila sababu za
kuwagawanya lakini aliwatahadharisha wananchi kuepukana na propaganda
kama hizo kwani zinaweza kuitia nchi katika pahala pabaya na kutoweka
kwa amani.
“Sisi
hatuhusiki na waraka huo aliyetoa waraka huo ni watu ambao wanapingana
na amani iliyopo lakini pia ni watu wenye kueneza propaganda mbaya za
kutaka kuwagawa wazanzibari jambo ambalo sisi tunaamini hatuna ugomvi na
wazanzibari wote sisi ni dugu hatubagui awe ni mkristo au muislamu awe
mweupe au mweusi hatuwezi kubaguana kwa kuwa misingi ya dini yetu
imekataza kubaguana” alisema Azzan.
Dereva wa Sheikh Farid aongea
Akizungumzia
mkasa wa kupoteza kwa Sheikh Farid, Dereva aliyempakia, Said Omar
alisema alitumwa kununua na kupeleka umeme nyumbani kwao na ndipo
alipomuacha Sheikh huyo hapo eneo la Mweni hapo akiwa na watu
wakizungumza naye ndani ya gari aina ya Noah lakini hakuwahi kuchukua
namba zake na pia hakuweza kuona sura za watu hao kwa kuwa walikuwa
katika gari yenye vioo vyeusi.
Akizungumza
kwa khofu mbele ya waandishi wa habari huko Mbuyuni Mjini Unguja, muda
mfupi baada ya kumaliza sala ya Ijumaa Said alisema kwamba baada ya
kurejea nyumbani alimfuata ambapo hakumkuta tena jambo ambalo lilimtia
wasiwasi na kurejea kuongea na wake zake nyumbani kwamba Sheikh Farid
haonekani.
Naye
kwa upande wake Naibu Amir wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya
Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) Azzan Khalid Hamad anasema taasisi za
kiislamu zinaamini kwamba Sheikh Farid bado yupo mikononi mwa jeshi la
polisi.
Sheikh
Azzan alisema bado wataendelea kumtafuta licha ya kuwa serikali
inaonekana kushindwa kufanya hivyo ambapo wametoa wametoa muda wa saa 26
hadi hapo kesho iwapo hajaonekana watachukua hatua wenyewe ya
kumtafuta. Aidha
aliwataka waumini wa dini ya kiislamu kuendeleza amani katika kipindi
hicho na kuacha kujiingiza katika makundi ya kihuni ambapo alisema
kumetokea vijana wenye kufanya vurugu na baadae kusingiziwa Uamsho.
Sheikh
Azzan alisema kukamatwa kwa Sheikh Farid ni juhudi za kuwarejesha nyuma
wazanzibari katika kudai haki yao ambapo alisema wapo watu ambao
hawataki kuona serikali ya umoja wa kitaifa ikiendelea na ndio wanafanya
kila njia ya kuvuruga amani nchini.
Chuo cha ICPS Mwembeladu chaharibiwa
Wakati
hali ya usalama katika maeneo mbali mbali haijatulia na mali na
miundombini kuharibiwa, vijana wenye kuendesha vurugu wamevamia chuo
kimoja cha ICPS kilichopo maeneo ya Mwembeladu na kuvunja vunja jengo
lao na vifaa viliyomo ndani.
Akizungumza
na Mwananchi Mkuu wa chuo hicho, Omar Othman alisema awali waliona
kundi la vijana likisonga mbele na kufika katika chuo hicho na kutaka
kuingia ndani baada ya kuvunja milango na madirisha na kisha kuiba vitu
mbali mbali katika chuo hicho.
Baraza la Wawakilishi.
KUFUATIA machafuko
yalioibuka kwa siku ya tatu mfululizo jana Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) waligoma kuingia katika
baraza hilo ili kuishinikiza serikali kuchukua hatua za haraka za
kumaliza machafuko na kurejesha hali ya usalama Zanzibar.
Wajumbe wa baraza hilo
ambao hawana nyadhifa serikalini kutoka kambi ya CCM “Backbanchers”
walianza mgomo wao juzi jioni na kususia vikao vya Baraza la Wawakilishi
vinavyoendelea na jana asubuhi kulazimika Spika wa baraza hilo, Pandu
Ameir Kificho kuahirisha kikao kwa muda wa dakika tano ili kutoa fursa
ya wajumbe hao kujipanga na kurudi ndani ili shughuli za baraza
ziendelee.
Jumla ya wajumbe wa baraza
hilo wote ni 82 pamoja na Spika na shughuli zote za baraza hilo
zinahitaji kuendelea kwa kuwa na nusu ya wajumbe ambapo wajumbe
waliokuwepo awali walikuwa ni 24 jambo ambalo lilifanya baraza hilo
kusiktisha shughuli zake kwa muda ili kutoa fursa ya kuwashawishi
wajumbe waliogoma waingie ndani na kuendeleza shuguli hizo ambapo Waziri
wa Afya, Juma Duni Haji alikuwa anahitaji kupata idadi ya wajumbe
waliotimiza koramu ili kupitisha muswada wake aliouwasilisha.
Kwa mujibu wa Mnadhimu wa
CCM ndani ya Baraza la Wawakilishi, Salmin Awadh Salmin, wajumbe kutoka
chama hicho wamefikia uamuzi huo wa kugomea vikao kutokana na vurugu
zinazoendelea na kutaka Spika akubaliane na hoja binafsi ya kujadili
hali ya kisiasa Zanzibar jambo ambalo Spika alikataa.
Hata hivyo, baada ya
mashauriano kati ya viongozi serikali, Spika na wajumbe hao wa CCM
walikubali kurudi na kuendelea na vikao ambapo walikuwa wajumbe 45 huku
wakishutumu kuwa serikali ya Zanzibar imeonesha udhaifu mkubwa katika
kuwahakikishia wananchi wake usalama na kuwataka Mkuu wa Jeshi ya Polisi
nchini IGP, Said Mwema pamoja na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali
Mussa kuwajibika kwa madai kwamba wameshindwa kutekeleza wajibu wao na
kuacha hali tete ya usalama ikiendelea.
Wakizungumza na waandishi
wa habari wajumbe hao walisema kwamba hali inavyoendelea inatishia
usalama wa serikali ya maridhiano na hivyo kuitaka serikali kuifuta
jumuiya ya Uamsho kwani wamekuwa wakiendeleza vitendo vya uvunjifu wa
amani bila ya kuchukuliwa hatua yoyote.
Shughuli za Baraza
zilianza tena baada ya Spika kutoa nasaha na kuwataka wajumbe hao
kuzingatia ahadi za kuwatumikia wananchi pamoja na Serikali ya Umoja wa
Kitaifa.
Vurugu zilizoanza Jumatano
baada ya kutoweka kwa kiongozi wa taasisi za Kiislamu, Sheikh Farid
Hadi Ahmed ambaye hadi sasa hajaonekana huku harakati za kijamii
zikikwama katika maeneo mbali mbali ikiweno wanafunzi kushindwa kupata
utulivu katika mitihani ya kidatu cha nne ambapo bado hofu imetanda
miongoni mwa wananchi.
Post a Comment