ALEX FERGUSON, RAFAEL BENITEZ WAANZA MALUMBANO

LONDON, England

“Benitez ana bahati sana kwa sababu CV yake ndani ya wiki mbili inaweza kuwa na mataji mawili ya ubingwa wa dunia ngazi ya klabu. Alifanya hivyo akiwa na Inter Milan iliyoachwa na Mourinho – wakati hakuna alichofanya kufanikisha hilo akiwa na timu”

SIKU mbili tangu Rafael Benitez alipotangazwa kuwa kocha wa kuinoa Chelsea, vita kali ya maneno imeibuka kati yake na Sir Alex Ferguson wa Manchester United.

Ni vita iliyozinduliwa na tamko la Fergie, kuwa kocha huyo mpya Darajani, ana ‘bahati’ kupata nafasi ya kufanya kazi Chelsea, na kwamba yuko katika nafasi kubwa ya kuboresha CV yake bila kufanya kazi yoyote.

Ndipo Mhispania huyo alipofura kwa hasira na kumjibu, huku akimuonya Msakochi huyo kwa kumwambia: “Usinishinikize.”

Benitez anatarajia kuiongoza kwa mara ya kwanza Blues leo Jumapili, katiika pambano la kukata na shoka la Ligi Kuu ya England kwa mechi dhidi ya Manchester City kwenye dimba la Stamford Bridge.

Kauli ya Fergie kuwa ana nafasi ya kuboresha CV bila kufanya kazi, inatokana na ukweli kuwa, anatarajia kuiongoza Chelsea kuwania Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia mwezi ujao huko nchini Japan – taji linalowaniwa na klabu bingwa za mabara.

Na katika hilo Fergie hakusita kusema: “Benitez amekuwa akihaha kusaka kazi ya muda mrefu.

“Ana bahati sana kwa sababu katika CV yake ndani ya wiki mbili inaweza kuwa na mataji mawili ya ubingwa wa dunia ngazi ya klabu – wakati hakuna chochote alichofanya kufanikisha hilo akiwa na timu hiyo.

“Jose Mourinho aliiwezesha Inter Milan kutwaa mataji matatu – alipoondoka Benitez akapata bahati ya kuinoa timu na kuiongoza kutwaa Klabu Bingwa ya Dunia wakati hakuna kazi yoyote aliyofanya,” alifunguka Fergie.

Kufuatia kauli hizo za Fergie, saa chache baadaye Benitez akiwa na hasira akajibu akisema: “Napendelea sana kuongea kuhusu timu na wachezaji wangu – lakini kama kuna watu wanajaribu kukushinikiza, nawe unapaswa kurejesha shinikizo kwao.

“Watu hujaribu kushinda katika njia tofauti. Napenda kuwaheshimu watu, lakini mara nyingine nashindwa kwa sababu baadhi yao wanakusukuma.

“Baadhi ya makocha hususani wa timu za katikati ya msimamo, wanaweza kuwa marafiki na yeyote. Lakini unapocheza ili kushinda ubingwa, kunakuwa na bingwa mmona tu, hivyo nitaipigania klabu yangu.

“Siwezi kusubiri wakati wao wakinisukuma na kunishikiza. Hivyo labda lazima nami nianze kurejesha msukumo na presha dhidi yao,” alisema Benitez bila kumtaja moja kwa moja Fergie.

Post a Comment

أحدث أقدم