Maadhimisho Kupinga Ukatili Dhidi Ya Wanawake


 Mkuu wa mkoa wa singida
 Kikundi cha nyota njema kikitumbuiza ngoma ya asili ya kabila la Kinyaturu wakati wa maadhimisho ya siku ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia

Na Elisante John;Singida
Novemba 28,2012.
 
SERIKALI imeyataka mashirika ya kiraia kushirikiana pamoja, ili kupiga vita na hatimaye kutokomeza kabisa vitendo vinavyosababisha ukatili wa kijinsia, hususani wanavyofanyiwa wanawake na watoto wadogo nchini.
 
Hayo yamebainishwa mjini Singida na mkuu wa mkoa huo, Dk. Parseko Kone, kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake, yaliyoadhimishwa kitaifa katika viwanja vya Peoples, mjini Singida, jana.
 
Maadhimisho hayo, yamefanyika mkoani Singida, kwa ushirikiano wa mashirika 16 hapa nchini, yaliyoipa dhamana ya kusimamia sherehe hizo, shirika la Action Aid-Singida,huku kauli mbiu yake ikiwa ‘FUNGUKA! Kemea ukatili dhidi ya wanawake, sote tuwajibike’.
 
Dk. Kone alisema kuwa, kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili wanawake ikiwemo ukatili wanaofanyiwa na wanaume, serikali kwa kushirikiana na mashirika ya kirai bado yanayo kazi kubwa katika kuungana pamoja ili kutokomeza unyanyasaji huo.
 
“Madhara yatokanayo na ukatili kwa wanwake katika jamii hupunguza nguvu kazi ya Taifa, baadhi ya madhara ya ukatili huo ni mauaji ya wanawake, ulemavu wa kudumu wa viungo…kupungua kwa uzalishaji kwa kuwa mwanamke ndiye mzalishaji mkuu kwenye kaya nyingi hapa nchini,”alisema Dk. Kone.
 
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, mkuu wa wilaya Singida mwalimu Queen Mlozi aliagiza kuwa ni vema sherehe kubwa kama hiyo inapofanyika mkoani hapa, wahusika wakashirikisha serikali ili iweze kufana zaidi.
 
Mwalimu Mlozi alilazimika kutoa amri hiyo, baada ya maadalizi, husani hamasa kuwa katika kiwango cha chini sana, hali iliyochangia uwanja kuonekana mtupu kutokana na watu wachache sana kujitokeza, vikiwemo vikundi vichache vya hamasa.
 
“Jamani ni vizuri maadhimisho makubwa kama haya yanapoletwa mkoani kwetu, basi wahusika wajitahidi kushirikisha serikali washirikiane pamoja kuhamasisha wananchi ili wajitokeze kwa wingi na wafurike kwenye sherehe,”alisema kwa masikitiko Mlozi.
 
Akizungumzia maadhimisho hayo, Juliana Bwire, afisa usawa na jinsi wa shirika la Concern worldwide kutoka jijini Dar es Salaam alisema siku 16 walizokuwa Singida, walizitumia vijijini kuielimisha jamii madhara ya ukatili, ikiwemo unyanyasaji, ukeketaji, na wanawake kunyimwa haki.
 
Aidha mmoja wa wanawake waliohudhuria sherehe hizo, Happynes Juma(30) mzaliwa wa Kigoma, alieleza kwa masikitiko ukatili aliofanyiwa na mumewe ikiwemo kudaiwa hajui kufanya mapenzi, hali iliyoleta mgogoro wa kifamilia na suala hilo lipo ustawi wa jamii, tayari kwa ajili ya kutengana.
 
Alisema maadhimsho hayo yatahitimishwa jijini Dar es Salaam siku ya desemba 8, mwaka huu

Post a Comment

Previous Post Next Post