
Akinamama wakicheza ngoma ya yailya katika jengo lililokuwa la Chifu Merere Mgandilwa wa Usangu kwenye Kijiji cha Mbalino.
Mgogoro wapamba moto katika Himaya ya Uhehe
HUU ni mfululizo wa Makala ya Uchunguzi
kuhusiana na historia ya kiongozi mkuu wa Wahehe, Chifu Mkwavinyika Munyigumba
Kilonge Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa, kama yanavyoandikwa na Mwandishi Wetu
DANIEL MBEGA, ambaye amefanya uchunguzi kwa takriban miezi mitatu sasa katika
kuhimiza utalii wa ndani na kuhifadhi historia yetu. Endelea na Sehemu hii ya
Nane…
KAMA tulivyoona huko nyuma, Wajerumani walionekana wema kuliko Mkwawa, ambapo
makabila mengi yaliyoizunguka Himaya ya Uhehe yaliyokuwa yakinyanyaswa hapo
kabla yaliona kwamba Wazungu hao ndiyo kimbilio lao na wangeweza kuwatetea
dhidi ya Mkwawa.
Wazungu kwa kiasi
kikubwa wanaipotosha historia katika kuhalalisha kile wanachodhani Waafrika
watakiona ndicho bora zaidi. Katika historia ya Mkwawa, wanadai kwamba, utajiri
ambao Chifu Mkwawa aliurithi kutoka kwa baba yake Munyigumba ulikuwa ni wa
dhulma, kwamba waliupata kwa kupora misafara, kama walivyofanya Wangoni na
Wasangu.
Na itakumbukwa kwamba,
Mkwawa aliendelea kuivamia misafara ya Wajerumani katika Njia ya Kati kadiri
alivyoweza, hali ambayo baadaye ikasababisha mapigano mengine katika Kijiji cha
Munisagara Desemba 7, 1892 ambapo pamoja na Wahehe kushindwa, lakini
walifanikiwa kukiteketeza Kijiji cha Kondoa kwenye Bonde la Mukondoa karibu na
ngome ya Wajerumani ya Kisaki.
Lakini siyo siri kwamba, ushindi wa Wahehe dhidi ya Wajerumani Agosti
1891 ulisikika kila pembe ya Afrika Mashariki ambapo Waafrika waliuzungumzia
sana. Lakini mwishoni mwa mwaka 1892 na mwanzoni mwa 1893 kulikuwa na kila
dalilia kwamba Wajerumani wangeweza kutawala kwa sababu nguvu zao dhidi ya
Wahehe zilikuwa zimeimarika na kutanua mpaka wao.
Wasagara, ambao awali walikuwa wameishi kwa hofu ya Mkwawa na kumpelekea
zawadi kila wakati ili asiwapige, sasa waliishi jirani na kambi za Wajerumani
na wakaanza kuubeza uwezo wa Wahehe waziwazi.
Itaendelea...www.kwanzajamii.com/?p=4487
إرسال تعليق