Tume ya Mabadiliko
ya Katiba inatarajia kuendelea na awamu ya nne na ya mwisho ya mikutano yake na
wananchi wa mikoa sita kuanzia siku ya Jumatatu, Novemba 19, 2012 hadi Jumatatu,
Desema 19, 2012 kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba
Mpya.
Mikoa hiyo ni Dar es
Salaam, Arusha, Simiyu, Geita, Mara na Mjini Magharibi na kila siku kutafanyika
mikutano miwili, wa kwanza utaanza saa 3:00 asubuhi – saa 6:00 mchana na
kufuatia na mwingine utakaoanza saa 8:00 alasiri – saa 11:00 jioni.
Taratibu zote za
kuanza kazi ya kukusanya maoni katika mikoa iliyotajwa zimekamilika zikiwemo
kuandaa ratiba na kuisambaza katika ofisi za mikoa, wilaya na Halmashauri za
Manispaa na Wilaya husika. Wajumbe wa Tume na watumishi wa Sekretarieti
wamejigawa katika makundi saba. Kila mkoa utakuwa na kundi moja isipokuwa Dar es
Salaam ambao utakuwa na makundi mawili.
Katika mkoa wa Dar
es Salaam Tume imejigawa katika makundi mawili na siku hiyo ya Jumatatu itaanza
na Wilaya za Temeke na Ilala. Katika wilaya ya Temeke, Tume itaanza na eneo la
Keko wakati katika wilaya ya Ilala itaanza na eneo la Jangwani kwa mikutano
itakayoanza saa 3:00 asubuhi. Kwa mikutano ya alasiri, wilayani Temeke mkutano
huo utafanyika Chang’ombe na ule wa Ilala utafanyika
Tabata.
Kwa upande wa mkoa
wa Arusha, Tume itaanza na Wilaya ya Karatu eneo la Mbulumbulu wakati mkoani
Mara Tume itaanza katika Wilaya ya Tarime eneo la Bumera. Kwa mkoa wa Simiyu,
Tume itaanza na Wilaya ya Busega eneo la Lamadi na mkoani Geita, Tume itaanza na
Wilaya ya Chato eneo la Kachwamba. Kwa mkoa wa Mjini Magharibi, Tume itaanza
katika Wilaya ya Magharibi.
Tume inawaomba
wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na kushiriki kikamilifu
katika kutoa maoni yao kwa kuzungumza na pale wanapokosa nafasi ya kuzungumza,
watumie fursa ya kuwasilisha maoni yao kwa maandishi kwa kutumia fomu maalum
zitakazokuwa zinatolewa na Tume katika mikutano
hiyo.
Pamoja na
kuwasilisha maoni kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume, wananchi pia wanaweza
kuwasilisha maoni yao kupitia tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) au kwa njia
ya posta kupitia anuani za zifuatazo:
i.
Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Makao Makuu, Mtaa wa Ohio, S.L.P. 1681, DAR ES SALAAM, Simu:
+255 22
2133425, Nukushi: +255 22 2133442; Au
ii.
Jengo la Ofisi ya
Mfuko wa Barabara, Mtaa wa Kikwajuni Gofu, S.L.P. 2775, Zanzibar, Simu: +255 224
2230768, Nukushi: +255 224 2230769
Tume inawaomba
wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na kushiriki kikamilifu
katika kutoa maoni yao kwa uwazi, uhuru na
utulivu.
إرسال تعليق