.jpg)
WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania
(Tanroads), kuanza kuvunja nyumba zilizopo ndani ya hifadhi ya Barabara
ya Mwenge hadi Morocco, Dar es Salaam ili kupisha ujenzi wa barabara nne
za lami.
Pia, ameitaka Tanroads kuacha kigugumizi katika ujenzi wa barabara za
juu jijini Dar es Salaam (flyovers) kwa kuwa fedha kwa ajili ya kazi
hiyo zipo.Waziri Magufuli alitoa wito huo Dar es Salaam jana, alipokuwa
akizindua bodi mpya ya Mfuko wa Barabara na Bodi ya Tanroads.
“Barabara ya Mwenge- Morocco nyumba zinatakiwa kubomolewa. Zibomolewe
haraka ili kupisha ujenzi. Nasema Tanroads acheni kigugumizi kwenye
masuala haya,” alisisitiza Dk Magufuli.
Ingawa hakuzianisha nyumba zilizotakiwa kubomolewa katika barabara hiyo,
sehemu kubwa ina nyumba za thamani kubwa hasa ghorofa jambo ambalo
linatarajiwa kuwaweka katika wakati mgumu wamiliki wake.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema:
“Nyumba zitakazobomolewa siyo nyingi. Ni zile zilizojengwa ndani ya mita
30 ya hifadhi ya barabara. Kinachotuchelewesha ni kuondolewa kwa nyaya
za umeme pamoja na mfumo mkubwa wa maji ili tuweze kuanza ujenzi.”
Waziri Magufuli alisema fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo zipo
na hata za kuwalipa wamiliki wa nyumba hizo zipo, hivyo akasisitiza kuwa
kazi ya kuzibomoa inapaswa kuanza mara moja.
“Wanaostahili kulipwa fidia walipwe na ambao hawastahili waondoke. Suala
la kwamba mko kwenye mchakato life na libaki kuwa neno la wanasiasa
tu,” alisema Magufuli.
Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2012/13, imeonyesha kuwa
barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 4.3, ujenzi wake unafadhiliwa na
Serikali ya Japan.
Kuhusu ujenzi wa barabara za juu, Waziri Magufuli alisema ni jambo linalowezekana na halihitaji kufanyiwa mchakato wowote.
Alisema ni muhimu bodi hiyo mpya ikasimamia ujenzi wa barabara hizo ili kupunguza msongamano wa magari Dar es Salaam.
“Tengenezeni ‘flyovers’ nyingi nyingi, ni kazi ndogo lakini inashangaza
kwa nini Tanroads inakuwa na kigugumizi,” alisema Magufuli na kuongeza:
“Wahandisi wa Tanroads fanyeni hivyo, mbona kule Kenya mambo yamefanyika
bila tatizo? Acheni kigugumizi na siasa mfanye kazi.”
إرسال تعليق