YUMKINI
hakuna shabiki hata mmoja wa sanaa ya maigizo, filamu na komedi hapa
nchini, asiyelifahamu jina la nguli wa tasnia hiyo, Said Ngamba ‘Mzee
Small’.
Hiyo
ni kwasababu, Small ni kati ya wakongwe waliotokea kuzizolea sifa
kemkemu, kutokana na umahiri alionao katika kukonga nyoyo za watazamaji
wa muvi za Kibongo.
Kwa
wale waliokwishabahatika kutazama baadhi ya kazi alizowahi kushiriki
mkongwe huyo, akiwa katika husika yoyote ile, wanaweza kuwa mashahidi
wakubwa juu ya hilo.

Mzee Small akiwa Sebuleni kwake
Hivi
karibuni, Small alikubwa na zahama ya ugonjwa wa kupooza mkono pamoja
na mguu wake wa kusho, hali iliyosababisha kusimama wa shughuli zake
zote hivi sasa.
Ugonjwa
huo ulimpata ghafla katikati mwaka jana alipokuwa njiani wakati
akirejea kutoka jijini Mwanza katika mradi wa Vicky Mtetema, wa kusaka
walemavu wa ngozi (Maalbino), ili kuwapeleka nchini Marekani.
Akizungumza
na Saluti5 mapema wiki iliyopita, nyumbani kwake Tabata Mawenzi, Small
anasema kuwa, ana zaidi ya mwaka mmoja sasa hajatoka nje, huku familia
yake ikimfanyia kila kitu kama mtoto mdogo.
“Kiukweli,
nasikitika kuona hakuna msaada wowote ninaoupata kutoka kwa viongozi wa
serikali, licha ya kuwa kati ya waigizaji wa mwanzo, niliyechangia
mapinduzi makubwa kisanaa,” anasema Small.

Japo kapooza mguu, kusimama mwenyewe si jambo linalomsubua
Anasema
kuwa, hivi sasa amekuwa akikosa ushirikiano wa kutosha hata kwa wasanii
wenzie waliokataa kumkumbuka hata tu kwa kumsalimu kupitia simu yake ya
mkononi.
Hata
hivyo, kama ilivyo ada, penye wabaya halisi na wema pia hawakosi, kuna
baadhi ya wasanii ambao wamekuwa wakifika nyumbani kwake mara kwa mara
na kumjulia hali.
Anawataja
baadhi yao kuwa ni pamoja na ‘mke wake wa maigizo’ ‘Bi Chau’, Tupatupa,
Seif Mbembe, Kingwendu, Senga, Mhogo Mchungu, Natasha, JB, Dk Cheni na
timu ya wachekeshaji wa ‘Mizengwe’.
“Maisha yangu hivi sasa yamekuwa magumu mno, kutokana na kuwa, kama
ilivyo kwa walalahoi wengine wengi, riziki yangu iko miguuni, hivyo
kukaa kwangu kitako kumefunga mambo mengi,” anasema Small.
Anafafanua
kuwa, maisha yake yamekuwa magumu kwasababu, yeye ndio tegemeo kwenye
familia, kuanzia katika kulisha hadi kusomesha wanawe ambao wengine wako
elimu ya juu.
Small
anawaomba wasanii wenzake, mashabiki pamoja na wadau wa sanaa ya
maigizo kujitokeza kwa wingi kumsaidia, kutokana na kuwa, hana akiba
inayoweza kumwendeshea maisha yake.
Pamoja
na kusumbuliwa na maradhi hayo, bado Small anaamini kuwa iko siku Mungu
atamwinua na kuanza kuburudisha tena kwa kufyatua kazi nyingine zaidi
na kufanya maonesho.

Shida ni pale anapotaka kutembea, ni lazima asaidiwe
“Nanachosisitiza
zaidi ni dua za Watanzania wenzangu, ili nipate nafuu haraka na endapo
nitainukiwa, nitafanya onesho kubwa maeneo ya Jangwani, jijini Dar es
Salaam,” anasema Small.
Anasema
kuwa, kadhalika, atazunguuka mikoa mingine yote hapa nchini na
kutumbuiza akiwa na kundi lake Afro Dance, hiyo ikiwa ni moja ya nadhiri
kubwa alizoweka.
Akielezea
namna alivyojitumbukiza kwenye uigizaji, Small anasema kuwa, mwaka 1970
alijifunza kuigiza kwa mtu aliyemtaja kwa jina la Said Seif Unono
ambaye ni marehemu kwa sasa.
Hiyo
ni baada ya mwaka 1965 kutua jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza na
kufikia Mtaa Sukuma na Mafia, Kariakoo, akitokea kijijini kwao ambako
muda wote tangu azaliwe alikuwa akilima mazao mbalimbali ya chakula.
“Mwaka
1978 nilijiunga na Chuo cha Sanaa, Bagamoyo nikitokea kikundi cha Reli,
ambako nikiwa Bagamoyo nilijifunza kwa miezi mitatu, kabla ya mwaka
1980 kuingia kikundi cha Jeshi la Magereza,” anasema Small.
Anasema,
kuingia kwake Magereza alikoajiriwa na kupewa cheo cha Koplo, baada ya
kuhudhuria na kufuzu vema mafunzo ya kijeshi, kulkitokana na kuvutwa na
askari aitwaye Juma Futo.
Akiwa
na Magereza, Small anasema kuwa, aliweza kuonesha cheche zake katika
sanaa kiasi cha kutuzwa cheo cha Koplo na rais wa wakati huo, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere.
Miaka
miwili baadaye, yaani mwaka 1982 rigwaride lilimshinda Small, akaachana
na Magereza na kujiunga na kundi la Agizo Group lililokuwa chini ya
mwalimu wake, Unono.
“Baadaye
kodogo nikaingia kundi lililokuwa likitikisa vilivyo wakati huo,
Muungano Culture Troupe chini ya mkali wa kucheza na nyoka, Norbert
Chenga, ambako nilikuwa mwigizaji na mcheza ngoma pia,” anasema Small.
Mwaka
1990 alifungasha virago Muungano na kuamua kuanzisha kundi lake
aliloliita Afro Dance akiwa na wasanii kadhaa mahiri kama vile;
Tupatupa, Hamis Chau na marehemu Zabibu.
Kutokana
na fitna hizi na zile za kisanaa pamoja na kutojipanga kwake
kikamilifu, Afro Dance ilikufa muda mfupi baada ya kuliasisi, akaajiriwa
Bima Modern Taarab alikokutana na Bi Chau.
Bima
Modern iliposambaratika, alimchukua Chau na kufufua Afro Dance
linalotamba hadi sasa likiwa na filamu nyingi kali, zikiwamo zile za
hivi karibuni; ‘Piga Ua Talaka Utatoa’ na ‘Tanga Waja Leo Waondoka Leo’.
“Nashukuru
alhamdullilah sanaa imenijengea nyumba, kunisomeshea watoto, kuniolea
mke, kutembea hadi nje ya mipaka ya Afrika na kujuana na wengi npamoja
na kupata senti ya kula,” anathibitisha Small.
Hata
hivyo, Small bado analia na upendo kiduchu uliopo miongoni mwa wasanii
kwa kutothaminiana na kila mmoja hamjali mwingine ipasavyo.

Hii ndiyo nyumba ya Mzee Small
Unapomwulizwa
kama ana mpango wa kurithisha kizazi chake sanaa anayoifanya, Small
anasema mwanae yeyote anaweza kumrithi kwa mapenzi binafsi tu lakini si
kwa kujitolea kumfundisha.
Hivi
sasa, Small anapatikana muda wote nyumbani kwake, Tabata Mawenzi
anakoishi na mkewe na watoto wake sita, ambao ni Mhiddin, Yunus,
Mahmoud, Somoe, Sofia na Said.
Alizaliwa,
mwaka 1955, Mingumbi, Kililima na kupata elimu ya msingi katika shule
ya Mingumbi, ambako alisoma hadi darasa la tano, kati ya mwaka 1961 na
65.Wameandika jamaa wa www.saluti5.com
Post a Comment