MFUKO wa Taifa wa Taifa wa Afya
(NHIF) kesho unazindua rasmi mpango wa huduma za bima ya afya kwa
vikundi vya wajasiriamali ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti
wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete.
Uzinduzi huo utafungua milango
kwa vikundi mbalimbali kujiunga na huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo wafanyakazi wa Sekta
rasmi tu ndio walipewa nafasi ya kutumia huduma hizo.
Kwa mujibu wa Taarifa kwa umma
iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, inasema kuwa uzinduzi
huo utafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia saa 2.30 asubuhi.
Taarifa hiyo imesema kwamba
uzinduzi wa mpango huo unatoa fursa kubwa kwa Watanzania kuhakikisha
wanaingia kwenye utaratibu wa bima ya afya ili wawe na uhakika wa kupata
matibabu.
“Hii ni fursa nyingine
ambayo Mfuko imeona iitoe kwa Watanzania na hii inatokana na ukweli
kwamba huduma za matibabu zimekuwa zikipanda kila kukicha na
wananchi wengi kushindwa kumudu gharama hizo na wakati mwingine
kusababisha madhara makubwa yakiwemo ya kupoteza maisha…mtu akiwa kwenye
utaratibu wa bima anakuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote
hata kama hana fedha mfukoni,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Shughuli kubwa zitakazofanyika
katika uzinduzi huo ni pamoja na kuzindua huduma hiyo, kugawa
vitambulisho vya matibabu kwa wanachama wapya ambao wamejiunga kupitia
vikundi vya wajasiriamali vinavyoratibiwa na WAMA.

إرسال تعليق